Jumanne, 15 Novemba 2016

VIONGOZI WA SERIKALI WASHAURIWA KUTUMIA NDEGE ZA ATC
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu akionyesha mfano wa hati ya safari ya kuelekea Mwanza kupitia Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), kushoto kwake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu akiongea na waandishi wa habari kabla ya kufanya ziara ya kikazimkoani Mwanza kupitia Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), leo jijini Dar es salaam.Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipokea maoni kutoka kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa anga katika uwanja wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) wakati alipokagua utoaji wa huduma uwanjani hapo.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipokea maoni kutoka kwa wasafiri wanaotumia usafiri waa anga katika uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere wakati alipotembelea kukagua huduma zitolewazo uwanjani hapo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ndege Tanzania (ATCL) Eng. Ladislaus Matindi  akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati alipotembelea Uwanja wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) kukagua huduma zitolewazo uwanjani hapo.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa wahudumu wa ndege katika Chuo cha Shirika la ndege Tanzania (ATCL) alipotembelea kuona maendeleo ya chuo hicho.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Samia Suluhu amewasihi viongozi wa serikali na wananchi kutumia ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATC), ili kudumisha uzalendo na kuchangia pato la shirika hilo kwa lengo la kuhimili ushindani na kukuza uchumi wa nchi.

Ametoa rai hiyo jijini Dar es salaam alipopewa hati ya kusafiria kupitia ndege za shirika hilo wakati akisafiri na ujumbe wake kuelekea mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi.

“Napenda kutoa wito kwa viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla kutumia ndege zetu ili shirika letu lifanye kazi vizuri zaidi, kufanya hivi kutaongeza pato na kukuza uchumi wa nchi”, amesema Makamu wa Rais.

Ametanabaisha kuwa kwa kutumia ndege za Shirika la ATC kwa safari za ndani Serikali itaokoa fedha nyingi zinazotumika kwa kukodi ndege za mashirika binafsi.

“Mimi na ujumbe tumeamua kusafiri na ndege za shirika la ndege Tanzania kutokana na kubana matumizi, gharama tuliyotumia kwa safari hii ni shilingi Milioni saba na laki sita ambapo tungekodi ndege binafsi tungetumia milioni arobaini”, amefafanua Makamu wa Rais.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amempongeza Makamu huyo kwa kitendo cha uzalendo alichokionyesha na kutaka viongozi wengine wa Serikali na wananchi kwa ujumla kuiga mfano huo ilikuliinua shirika hilo na kuongeza uchumi.

“Nampongeza Makamu wa Rais kwa kuamua kutumia ndege za Shirika hili kwa safari za ndani, kitendo hiki kimeonesha nia ya dhati ya serikali ya kulifufua shirika hili, naomba wananchi nao waendelee kutumia ndege za shirika hili katika safari zao za ndani kama alivyofanya Makamu wa Rais”, amesema Waziri Mbarawa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mhandisi Ladislaus Matindi ameahidi kuboresha huduma katika shirika hilo ikiwemo mifumo ya kukatisha tiketi ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuvutia wateja wengi kwa lengo la kurudisha hadhi ya shirika.

“Tumeshaanza mchakato wa kuweka mfumo mpya wa kukatisha tiketi ikiwemo kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti ya shirika hili ambapo mteja hatalazimika kufika kwenye ofisi zetu”, amesema Mhandisi Matindi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni