Jumapili, 20 Novemba 2016

BARABARA YA NJOMBE-MAKETE-MBEYA KUWEKWA LAMI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mang’oto Wilayani Makete ambapo aliwataka walioko kwenye hifadhi ya barabara wabomoe nyumba zao na kutafuta nyumba mbadala ili kuwezesha zoezi la ujenzi wa barabara kuanza na zoezi la fidia lifuate baadaye.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo kwa wananchi wa Kata ya  Iwawa Wilayani Makete ambapo aliwataka walioko kwenye hifadhi ya barabara wabomoe nyumba zao na kutafuta nyumba mbadala ili kuwezesha zoezi la ujenzi wa barabara kuanza na zoezi la fidia litafuatia baadaye.

Mbunge wa Makete Profesa, Norman Sigala akifafanua jambo kwa wananchi wa Jimbo hilo kuhusu umuhimu wa kutafuta nyumba mbadala ili kupisha ujenzi wa barabara ya Njombe –Makete KM 109 utakaoanza hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi (kulia), akimshukuru Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani kufuatia hatua ya ujenzi wa daraja la Ruhuhu linalounganisha mkoa wa Njombe na Ruvuma.

Wananchi wa kijiji cha Mang’oto Wilayani Makete wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Hayupo pichani).

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng, Edwin Ngonyani amewataka wananchi waliowekewa alama za kubomolewa nyumba zao zilizopo pembezoni mwa barabara ya Njombe-Makete hadi Mbeya Km 205 waanze kuhama kwenye nyumba hizo ili kupisha zoezi la ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo Eng. Ngonyani amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wake itaanza wakati wowote kuanzia sasa mara baada ya kupatikana mkandarasi na mkandarasi mshauri ambayo itahusisha sehemu ya Njombe hadi Makete KM 109.4.

“Kuweni waadilifu waliowekewa alama za kijani kwenye nyumba zao watalipwa fidia lakini wenye alama nyekundu hawatalipwa hivyo ni vizuri wote kutafuta maeneo mengine ya makazi ili kuepuka usumbufu mara zoezi la ujenzi litakapoanza”. Amesema Eng. Ngonyani.

Eng. Ngonyani amesema kwa kuwa kazi ya ujenzi na ulipaji fidia zinagharamiwa na Serikali ni vema zoezi la ujenzi wa barabara likaanza wakati Serikali ikitafuta fedha kwa ajili ya fidia.
“Ili tuweze kufanikiwa katika mambo yote tumeona tuanze na zoezi lenye gharama kubwa ambalo ni ujenzi wa barabara kisha zoezi la fidia litaendelea wakati ujenzi wa barabara unaendelea”. amesisitiza Eng. Ngonyani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi wa daraja la Ruhuhu linalounganisha Mkoa wa Njombe na Ruvuma na ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuweka lami barabara inayokwenda kwenye hospitali ya Mkoa wa Njombe na ile inayoenda hospitali ya misheni ya Ikonda wilayani Makete ili kuwezesha barabara hizo kupitika kwa urahisi wakati wote wa mwaka.

Katika hatua nyingine Mbunge wa Makete Profesa, Norman Sigara amemuomba  Naibu Waziri Eng. Ngonyani  kuhakikisha Mkandarasi anayejenga barabara ya Njombe –Makete na Makete –Mbeya kupitia Kitulo anaanza kazi iyo kwa wakati ili kuongeza kasi ya wananchi kubomoa nyumba zao katika maeneo ya hifadhi ya barabara na hivyo kuunganisha kirahisi mkoa wa Njombe na Mbeya kwa barabara ya lami.

Naibu Waziri Ngonyani yupo katika ziara ya kukagua Miundombinu ya Barabara, Bandari na Mawasiliano katika mikoa ya Nyanda za juu 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni