Muonekano
wa Daraja la Furahisha mkoani Mwanza, ambalo linatarajiwa kukamilika mwazoni
mwa mwezi Januari mwakani. Ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80.
Serikali
imeanza ujenzi na upanuzi wa viwanja 11 ikiwa ni hatua ya kuendelea kuboresha
na kukuza usafiri wa anga hapa nchini.
Akizungumza
mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika
kiwanja cha ndege cha Mwanza, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa amesema kuwa kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 150
zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya upanuzi wa viwanja hivyo.
Ameongezeza
kuwa miradi itakayotekelezwa katika viwanja hivyo ni pamoja na ujenzi wa
majengo ya abiria na upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege.
"Maboresho
ya miundombinu ya viwanja vya ndege yatachochea ongezeko la pato la Taifa,
hivyo basi Serikali imeonesha nia ya dhati katika kuhakikisha usafiri huu
utakuwa ni wa uhakika na nafuu kwa wananchi”, amesema Profesa Mbarawa.
Aidha,
Waziri Prof. Mbarawa amevitaja baadhi ya viwanja hivyo kuwa ni kiwanja cha
ndege cha Shinyanga, Tabora, Sumbawanga, Kigoma, Mtwara, Songea na Iringa.
Kuhusu
ujenzi wa Jengo la kuongozea ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza,
Profesa Mbarawa amesema kuwa Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 7.6
kwa ajili ya kumlipa mkandarasi na msimamizi wa mradi huo ambao unatarajiwa
kukamilika mwezi Agosti mwakani.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA),
Salum Msangi amesema Mamlaka itaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja
vya ndege lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watanzania wanapata huduma
zilizo bora na kukuza pato la Taifa.
Ameahidi
kuendelea kutatua changamoto ya ndege hai wanaohatarisha uharibufu wa miundombinu
za injini za ndege katika uwanja huo ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha usalama wa
anga na watumiaji wake.
Naye,
Mkandarasi wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG),
anayejenga jengo hilo, Yuzhang Xiong, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa
kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kwani kwa sasa jengo limefika katika
hatua nzuri.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mbarawa ametembelea Daraja la Furahisha na barabara ya
makongoro hadi uwanja wa ndege yenye urefu wa kilomita tano na kusema
kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kupunguza foleni kwa watumiaji wa
vyombo vya moto na ajali kwa watembea
kwa miguu.
Aidha,
amefafanua mradi huo kuwa umegawanyika katika sehemu tatu ambapo kwa sasa
sehemu ya tatu ya mradi huo iliyoanza inahusisha upanuzi wa barabara ya Mwaloni
hadi Furahisha Mita725 na ujenzi wa barabara ya Pasiansi hadi Uwanja wa Ndege
(km 5) kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Prof.
Mbarawa amewataka wananchi kutunza na kulinda miundombinu hiyo ambapo Serikali
imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharamia utekelezaji wa miradi hiyo.
Amewaagiza
uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Mwanza kumsimamia mkandarasi
wa kampuni ya Nyanza Roads anayejenga barabara hiyo kujenga kwa kiwango kilicho
bora ili kuweza kushawishi Serikali kuwapatia tenda za miradi mengine.
Meneja
wa TANROADS, mkoa wa Mwanza, Eng. Marwa Rubirya amesema kuwa hadi sasa
utekelezaji wa mradi wa Daraja la Furahisha umefikia asilimia 80 ambapo ujenzi
wa daraja na ufungaji wa vyuma umekamilika na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi Januari.
|