Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
akizungumza na wajumbe wa bodi mpya ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA), mara baada ya kuizindua rasmi, jijini Dar es Salaam.
|
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Bodi mpya ya Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakikisha wanapata mwarobaini wa kudhibiti ongezeko
la wizi wa mitandao unaoendelea kukithiri hapa nchini.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa bodi hiyo, Prof. Mbarawa amesema watanzania wameibiwa kwa muda
mrefu kupitia njia ya ujumbe mfupi na kushawishiwa kutoa fedha kwa njia ya
udanganyifu na hivyo kuitaka bodi hiyo kutofumbia macho changamoto hiyo.
“Changamoto ya wizi wa
mitandao inagusa watanzania wengi, mkiwa na jukumu la kudhibiti mna wajibu wa
kuwalinda wananchi”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa bodi
hiyo ihakikishe inasimamia kwa karibu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa
katika kudhibiti ubora wa masuala ya mawasiliano ikiwa ni teknolojia inayokuwa
kwa kasi kubwa.
Aidha Prof. Mbarawa
ameitaka bodi hiyo kuendelea kudhibiti wimbi la meseji za uchozezi zinazotumwa
na baadhi ya wananchi kwa kukosa maadili.
Katika kuimarisha
huduma ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini Waziri Prof. Mbarawa
ameikata TCRA kufanya maamuzi ya haraka na kuwa wabunifu ili kuweka mazingira
endelevu ya kukuza sekta hiyo.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt.
Faustine Kamuzora amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ataisimamia bodi
hiyo kwa kuzingatia ubora na kasi ya ukuaji wa teknolojia.
“Usipokuwa mbunifu
katika sekta ya mawasiliano unaweza kujikuta unadhibiti teknolojia iliyopitwa
na wakati hivyo ni lazima tuende sambamba na mabadiliko”, amesisitiza Prof.
Kamuzora.
Naye, Mwenyekiti wa
Bodi mpya ya TCRA Dkt. Jones Kilimbe amesema kuwa pamoja na changamoto
mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, Bodi itahakikisha inapata suluhu ya
changamoto hizo ndani ya muda mfupi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni