Jumatano, 24 Mei 2017

PROF. MBARAWA AITAKA BODI YA DMI KUBORESHA MIUNDOMBINU

Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.Serikali imeitaka Bodi ya Chuo Cha Bahari Dar es Salaam (DMI), kuhakikisha inaboresha miundombinu ya chuo na kuzingatia miiko na kanuni za ufundishaji ili wanafunzi wanaohitimu  chuoni hapo waweze kukidhi mahitaji ya soko. 


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema hayo leo jijini Dar es salaam, wakati akizindua bodi hiyo na kusisitiza kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha majengo kwa kutangaza zabuni kwa uwazi ili kuepuka mianya ya rushwa.

“Hakikisheni mnakuwa na mpango madubuti wa kuboresha majengo ya chuo ili chuo kibaki na hadhi yake, lakini pia hakikisheni  mntoa elimu bora kwa wanafunzi wanaokuja  kusoma hapa  ili waweze kupata misingi imara itakayowawezesha kuajiriwa ndani na nje ya nchi mara baada ya kuhitimu masomo  yao”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa Serikali ina uhitaji wa wataalam wengi kwenye masuala ya bahari hivyo ni wajibu wa bodi kusimamia chuo na kuhakikisha wataalam hao  wanazalishwa  kwa wingi chuoni hapo ili kukidhi mahitaji  ya soko kitaifa na kimataifa.

Amewataka wakufunzi wa chuo hicho kuhakikisha wanatumia lugha nzuri kwenye ufundishaji ili kuwaweka wanafunzi karibu na kuhakikisha wanapata taaluma inayotakiwa kwani kuwepo kwa waalimu hao kunategemea kuwepo kwa wanafunzi.

“Ni lazima tufungue milango kwa wanafunzi sababu wapo wanaoelewa haraka na  wanaoelewa taratibu, hivyo tukae nao muda mrefu ili kubaini changamoto zao lakini pia tuwe waangalifu juu ya matumizi ya lugha tunazotumia kwa wanafunzi wakati tunapofundisha”, amefafanua Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya DMI, Kapteni Ernest Bupamba,  amemuahidi Waziri huyo kuwa watafanya kazi ya kusimamia chuo hicho kwa juhudi zote na kwa maarifa yote ili chuo kizalishe wataalam wenye sifa kwenye sekta ya uchukuzi.

“Naahidi kushirikiana vyema na Wajumbe wezangu wa bodi, Menejimenti ya Chuo na watumishi katika utekelezaji wa majukumu ili kuleta tija", amesisitiza Kapteni Bupamba.

Aidha, Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Erick Massami amemuomba Waziri Mbarawa kukisaidia chuo hicho kuanza kutumia fedha za mfuko wa Usafirishaji ambazo zimekusanywa tangu mwaka 2013 bila kutumika ili fedha hizo zitumike kuzalisha wataalam wengi katika sekta ya usafiri  wa majini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua bodi ya chuo ambayo iko chini ya uenyekiti wa Kapteni Ernest  Bupamba  na wajumbe wanne ambao ni Kapteni Andrew Matilya, Dkt. Mwamini Tulli, Bi Tumaini Silaa na Eng. Alfred Waryana.

Jumatatu, 22 Mei 2017

TAARIFA YA UTEUZI


NAIBU WAZIRI NGONYANI AWATAKA MAKANDARASI BARABARA YA MAFINGA-IGAWA KUONGEZA KASI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akipitia taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Mafinga –Igawa sehemu ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 Mkoani Iringa mara baada ya kukagu mradi huo kulia ni Meneja Mradi huo Richarad Guo akisisitiza jambo.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akipata maelezo kutoka kwa Meneja Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mafinga –Igawa sehemu ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 Richarad Guo alipokagua ujenzi huo Mkoani Iringa.


Muonekano wa barabara ya Mafinga –Igawa sehemu ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 ambapo tayari Kilomita 18 zimekamilika kwa kiwango cha lami, ujenzi huo unafanywa na kampuni ya China Civil Engenering Construction Corporation (CCECC).


Mafundi wanaojenga barabara ya Mafinga-Igawa  sehemu ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 Mkoani Iringa wakiendelea na ujenzi wa karavati kubwa katika eneo chepechepe maarufu Majinja wilayani Mufindi.


Muonekano wa Mtambo wa kusaga kokoto pamoja na shehena ya kokoto zinazotumika katika ujenzi wa barabara ya Mafinga –Igawa.


Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amemtaka mkandarasi China Civil Engeneer Construction Cooporation (CCECC), anayejenga barabara ya Mafinga-Nyigo km 74.1 na (CRSG) anayejenga sehemu ya Nyigo –Igawa KM 63.8 kuongeza kasi ya ujenzi ili upanuzi na uimarishaji wa barabara hiyo ukamilike kwa wakati.


Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo Eng. Ngonyani amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole kuhakikisha upana wa barabara hiyo na ubora wake unakidhi malengo ya Serikali ili barabara hiyo ili idumu kwa muda mrefu na kupunguza msongamano na ajali zinazoepukika. 


“Barabara hii ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM inaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Zambia na Malawi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hivyo ni lazima isimamiwe kikamilifu ili idumu kwa muda mrefu”, amesisitiza Eng. Ngonyani.


Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole amesema tayari kilomita 18 kati ya 74.1 katika sehemu ya kwanza ya Mafinga –Nyigo imeshawekwa  lami na Mkandarasi ameunda timu tatu ili kuharakisha ujenzi huo. 


“Ujenzi wa barabara ya Mafinga -Igawa unahusisha mikoa mitatu ambapo Kilomita 74.1 ziko katika mkoa wa Iringa Mafinga-Nyigo, Kilomita 52 ziko katika mkoa wa Njombe Nyigo-Halali na Kilomita 12 ziko katika Mkoa wa Mbeya Halali-Igawa hivyo mimi pamoja na wenzangu tumejipanga kuhakikisha barabara hii inakamilika Novemba mwakani kama ilivyopangwa”, amesisitiza Eng. Kindole.


Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo Sehemu ya Mafinga – Nyigo KM 74.1 Richard Guo amemhakikishia Naibu Waziri huyo kwamba kasi yao ya ujenzi ni nzuri na barabara hiyo imeimarishwa ili kukidhi mahitaji na itakamilika kwa wakati.


Zaidi ya shilingi bilioni 116 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza yaani Mafinga- Nyigo km 74.1 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia.