Profesa Makame
Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Serikali imeitaka
Bodi ya Chuo Cha Bahari Dar es Salaam (DMI), kuhakikisha inaboresha miundombinu
ya chuo na kuzingatia miiko na kanuni za ufundishaji ili wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo waweze kukidhi mahitaji ya soko.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema hayo leo jijini
Dar es salaam, wakati akizindua bodi hiyo na kusisitiza kuweka mikakati
madhubuti ya kuboresha majengo kwa kutangaza zabuni kwa uwazi ili kuepuka mianya
ya rushwa.
“Hakikisheni
mnakuwa na mpango madubuti wa kuboresha majengo ya chuo ili chuo kibaki na
hadhi yake, lakini pia hakikisheni mntoa
elimu bora kwa wanafunzi wanaokuja kusoma hapa
ili waweze kupata misingi imara itakayowawezesha kuajiriwa ndani na nje
ya nchi mara baada ya kuhitimu masomo
yao”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa
Serikali ina uhitaji wa wataalam wengi kwenye masuala ya bahari hivyo ni wajibu
wa bodi kusimamia chuo na kuhakikisha wataalam hao wanazalishwa kwa wingi chuoni hapo ili kukidhi
mahitaji ya soko kitaifa na kimataifa.
Amewataka
wakufunzi wa chuo hicho kuhakikisha wanatumia lugha nzuri kwenye ufundishaji
ili kuwaweka wanafunzi karibu na kuhakikisha wanapata taaluma inayotakiwa kwani
kuwepo kwa waalimu hao kunategemea kuwepo kwa wanafunzi.
“Ni lazima
tufungue milango kwa wanafunzi sababu wapo wanaoelewa haraka na wanaoelewa taratibu, hivyo tukae nao muda
mrefu ili kubaini changamoto zao lakini pia tuwe waangalifu juu ya matumizi ya lugha
tunazotumia kwa wanafunzi wakati tunapofundisha”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya DMI, Kapteni Ernest Bupamba, amemuahidi Waziri huyo kuwa watafanya kazi ya
kusimamia chuo hicho kwa juhudi zote na kwa maarifa yote ili chuo kizalishe
wataalam wenye sifa kwenye sekta ya uchukuzi.
“Naahidi
kushirikiana vyema na Wajumbe wezangu wa bodi, Menejimenti ya Chuo na watumishi
katika utekelezaji wa majukumu ili kuleta tija", amesisitiza Kapteni Bupamba.
Aidha, Mkuu wa
Chuo hicho Dkt. Erick Massami amemuomba Waziri Mbarawa kukisaidia chuo hicho kuanza
kutumia fedha za mfuko wa Usafirishaji ambazo zimekusanywa tangu mwaka 2013
bila kutumika ili fedha hizo zitumike kuzalisha wataalam wengi katika sekta ya
usafiri wa majini.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua bodi ya chuo ambayo
iko chini ya uenyekiti wa Kapteni Ernest Bupamba
na wajumbe wanne ambao ni Kapteni Andrew Matilya, Dkt. Mwamini Tulli, Bi
Tumaini Silaa na Eng. Alfred Waryana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni