Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa safari za ndege za kampuni hiyo mkoani Tabora, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, amesema kuwa kuanzishwa kwa safari hizo katika mikoa hiyo
kutatanua wigo wa kibiashara na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo za utalii na kilimo.
“Naamini
wananchi wa mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani, sasa mtanufaika kwa ujio wa
ndege hii, matumaini yangu kwamba mtatumia usafiri huu ambao hautumii muda
mrefu katika kurahisisha shughuli zenu za kibiashara na kijamii”, amesema Eng.
Ngonyani.
Aidha,
Naibu Waziri Ngonyani amewataka wananchi wa mkoa wa Tabora kutumia fursa ya
ujio wa ndege hiyo kama chachu ya kuleta maendeleo katika mkoa huo.
Sambamba
na hilo Eng. Ngonyani, amesema kuwa katika kuhakikisha usafiri wa anga
unaimarika nchini Serikali itaongeza ndege nyingine tatu katika mwaka wa fedha
2017/18 ambapo hadi kufikia mwezi Julai mwakani ndege hizo zitakuwa zimewasili.
Naibu
Waziri Ngonyani amefafanua kuwa ndege mbili kati ya hizo zitakuwa za masafa ya
kati aina ya CS 300 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja na ndege
moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba
abiria 262.
Katika
hatua nyingine, Eng. Ngonyani amewaagiza wafanyakazi wa ATCL kufanya kazi kwa
juhudi, uadilifu na weledi kwa lengo la kuijengea sifa kampuni hiyo na kuvutia
wateja ili kujiimarisha katika soko la ushindani.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard
Chamuriho, amewataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya kupata usafiri wenye
gharama nafuu na wa muda mfupi.
Naye,
Mkuu wa Mkoa huo Bw. Aggrey Mwanri, amewataka wananchi wa mkoa huo na mikoa ya
jirani kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya usafiri huo ambao walikuwa
wakiusubiri muda mrefu.
Uzinduzi
wa safari za ndege mkoani humo ni moja ya hatua za kuboresha usafiri wa anga
nchini ambapo Serikali kupitia ATCL ina mpango wa kuanzisha safari katika mikoa
mingine na nchi jirani ili kurahisisha huduma za kijamii na kibiashara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni