Akizungumza hayo mjini Dodoma mara
baada ya kukagua Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light) zilizofungwa
uwanjani hapo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa, amesema kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa uboreshaji wa uwanja huo
katika kuruhusu ndege za aina zote kutua masaa 24 kwa wiki.
“Hii ni hatua ya pili ya
uboreshaji wa uwanja huu ambapo hatua ya kwanza tumeimaliza ya upanuzi wa
barabara za kuruka na kutua ndege (runway) hadi kufikia KM 2.5”, amesema Waziri
Profesa Mbarawa.
Aidha, ameongeza kuwa ufungaji
wa taa hizo umegawanywa kwa hatua tatu ambapo awamu ya kwanza imekamilika kwa
kujumuisha ufungaji wa Mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar
Powered Light), katika barabara za kuruka na kutua ndege na maeneo ya maegesho,
hatua ya pili ni kufunga taa za kumsaidia Rubani kuweza kuona uwanja wote na
hatua ya mwisho ni taa zitakazofungwa mita 400 kila upande uwanjani hapo.
Amefafanua kuwa Taa hizo za
kisasa (Aviation Solar Powered Light) zitapunguza gharama za uendeshaji
uwanjani hapo ikiwemo matengenezo yake kwani zinadumu muda mrefu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho, amesema kuwa nia ya Serikali
ni kuendelea kurefusha uwanja huo ambapo italipa fidia kwa nyumba zilizopo
pembeni ya uwanja huo ili kuongeza usalama wa uwanja na ndege kwa ujumla.
“Tutaweka uzio katika uwanja huu
kulingana na matakwa ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na pia kupitia uzio huu
taa zitakuwa salama”, amesisitiza Dkt. Chamuriho.
Naye, Msimamizi wa mradi Bw.
Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), amesema mfumo wa
taa hizo za kisasa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zimefungwa kwa
siku 14 na zina uwezo wa kufanya kazi kwa miaka 12 na kuwaka kwa masaa laki
moja ukilinganisha na nyingine ambazo zinawaka kwa masaa elfu kumi.
Mfumo wa uwekaji Taa za Kisasa ni
mkakati wa Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuboresha viwanja vyake vya
ndege ili kukidhi viwango vianavyostahili katika usafiri wa anga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni