Jumanne, 13 Juni 2017

TPA WASAINI MKATABA WA UPANUZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Prof: Makame Mbarawa akiongea na wadau wa sekta ya usafirishaji kabla ya zoezi la utiaji saini wa mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha Bandari kati ya Serikali na Kampuni ya China Harbour Engineering. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko na kushoto ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Bw. Mkinga Mkinga.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Prof: Makame Mbarawa (katikati) akishuhudia makabidhiano ya mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha Bandari kati ya Serikali na Kampuni ya China Harbour Engineering. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA). Mhandisi Deusdedit Kakoko na kushoto ni Mtedaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. XU XINPEI.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA). Mhandisi Deusdedit Kakoko kulia na Mtedaji Mkuu wa Kampuni ya China Harbour Engineering Bw. XU XINPEI wakionyesha mkataba wa makubaliano ya upanuzi na uongezaji wa kina cha Bandari kwa wadau wa sekta ya usafirishaji baada zoezi la utiaji saini wa mkataba huo kukamilika.


Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), imesaini mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha bandari utakaowezesha bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa za mizigo na kushindana na bandari nyingine katika pwani ya bahari ya hindi.


Upanuzi huo  utakaofanywa na kampuni ya China Harbor Construction  ya China utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 336 na utadumu kwa miezi 36, ambapo  utahusisha uongezaji wa kina cha lango la bandari na uongezaji wa kina cha maji kati ya gati namba 0, 1 hadi 7.


Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hatua hiyo inalenga kuifufua upya bandari ya Dar es Salaam ili ifanye kazi kwa ushindani na kuhudumia wateja wengi kuliko ilivyo sasa. 


“Kukamilika kwa upanuzi na uongezaji wa kina cha maji  katika gati namba 1 hadi 7 kutoka mita 8 hadi 15 kutawezesha meli kubwa na za kisasa zenye uwezo wa kubeba hadi makontena  elfu kumi na tisa kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa Tanzania”, amesema Prof. Mbarawa.


Aidha Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa pamoja na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya reli na barabara ili kuhakikisha mizigo haikai muda mrefu bandarini.


“Ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge toka Dare s Salaam hadi Kanda ya Ziwa na Kigoma na ufufuaji wa reli ya Tazara kutawezesha bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi kwa ufanisi na kuvutia wafanyabiashara wengi hivyo nawataka  wafanyakazi wote wa bandari kufanyakazi kwa bidii na uadilifu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko amesema kiasi cha dola za Marekani milioni 421, kitapatikana kwaajili ya ujenzi huo ambapo kati ya fedha hizo  Benki ya Dunia itatoa mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 345.


Kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa adha ya baadhi ya meli kusubiri kwa muda mrefu kupata nafasi ya kutia nanga na kutaongeza hadhi ya bandari ya Dar es salaam na kuvutia wasafirishaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Jumatano, 7 Juni 2017

WAZIRI MBARAWA APOKEA KIVUKO CHA MV KAZI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Bw. Major Songoro (kulia)  wakati wa makabidhiano ya Kivuko cha MV. KAZI mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Mtendaji Mkuu toka Wakala wa Ufundi na Umeme  (TEMESA) Dkt. Mussa  Mgwatu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kulia) akizungumza na baadhi ya wananchi waliopanda Kivuko cha MV. KAZI mara baada ya kukabidhiwa kwa Serikali toka kwa  Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Iliyokuwa ikikijenga Kivuko hicho.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliana Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akizungumza na mmoja  ya mkazi wa Kigamboni wakati wa kukabidhiwa kivuko cha MV. KAZI kwa Serikali toka kwa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Iliyokuwa ikikijenga Kivuko hicho.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akifurahia jambo na  mmoja  ya mkazi wa Kigamboni wakati wa kukabidhiwa Kivuko cha MV. KAZI kwa Serikali toka kwa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Iliyokuwa ikikijenga kivuko hicho.

Baadhi ya wananchi wakiteremka katika Kivuko cha MV. KAZI mara baada ya kukabidhiwa rasmi kwa Serikali mapema hii leo Magogoni jijini Dar es Salaam toka Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Iliyokuwa ikikijenga Kivuko hicho.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amepokea Kivuko cha MV Kazi kutoka kwa Kampuni ya kizalendo ya M/S Songoro Marine Transport Boatyard ya Mwanza iliyokuwa inafanya kazi ya ujenzi wa Kivuko hicho mara baada ya ujenzi wake kukamilika.

Akizungumza na wananchi, Prof Mbarawa alisema lengo la Serikali kuongeza Kivuko hicho  ni kuboresha huduma za kusafirisha abiria na magari kati ya Magogoni na Kigamboni.

“Uwepo wa vivuko vitatu kutasaidia utoaji wa huduma kwa wakati na kwa urahisi na ikitokea Kivuko kimoja kimepelekwa kufanyiwa ukarabati huduma zitaendelea kama kawaida bila kuathiri utaratibu wa kawaida”.Alisema Prof Mbarawa.

Ameongeza kuwa ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais John Magufuli  Wizara yake itaendelea kuboresha huduma za Vivuko katika Mikoa mingine ikiwemo Mkoa wa Lindi , Kivuko cha Pangani, na Kivuko cha Kigongo Busisi Mkoani Mwanza.

Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Dkt. Mussa Mgwatu alisema Kivuko cha MV Kazi kimejengwa kulingana na viwango vinavyotakiwa Kimataifa na ukaguzi wake umefanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa ubebaji wa abiria na magari.

 Ujenzi wa MV KAZI umegharimu Shilingi Bilioni 7.3 za Kitanzania na kina uwezo wa kubeba abiria 800 magari 22 sawa na jumla ya tani 170. 

Kivuko hicho kimekabidhiwa leo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni Jijini Dar es salaam na kuongeza idadi ya vivuko katika eneo hilo kufikia vitatu.