Baadhi ya wananchi wakiteremka katika Kivuko cha MV.
KAZI mara baada ya kukabidhiwa rasmi kwa Serikali mapema hii leo Magogoni
jijini Dar es Salaam toka Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Iliyokuwa
ikikijenga Kivuko hicho.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amepokea Kivuko cha MV Kazi kutoka kwa Kampuni
ya kizalendo ya M/S Songoro Marine Transport Boatyard ya Mwanza iliyokuwa inafanya
kazi ya ujenzi wa Kivuko hicho mara baada ya ujenzi wake kukamilika.
Akizungumza na
wananchi, Prof Mbarawa alisema lengo la Serikali kuongeza Kivuko hicho ni kuboresha huduma za kusafirisha abiria na
magari kati ya Magogoni na Kigamboni.
“Uwepo wa vivuko
vitatu kutasaidia utoaji wa huduma kwa wakati na kwa urahisi na ikitokea Kivuko
kimoja kimepelekwa kufanyiwa ukarabati huduma zitaendelea kama kawaida bila
kuathiri utaratibu wa kawaida”.Alisema Prof Mbarawa.
Ameongeza kuwa ili
kuendana na kasi ya Mhe. Rais John Magufuli
Wizara yake itaendelea kuboresha huduma za Vivuko katika Mikoa mingine
ikiwemo Mkoa wa Lindi , Kivuko cha Pangani, na Kivuko cha Kigongo Busisi Mkoani
Mwanza.
Nae Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Dkt. Mussa Mgwatu alisema Kivuko cha MV Kazi
kimejengwa kulingana na viwango vinavyotakiwa Kimataifa na ukaguzi wake
umefanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na
kuthibitishwa kuwa ni salama kwa ubebaji wa abiria na magari.
Ujenzi wa MV KAZI umegharimu Shilingi Bilioni
7.3 za Kitanzania na kina uwezo wa kubeba abiria 800 magari 22 sawa na jumla ya
tani 170.
Kivuko hicho
kimekabidhiwa leo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kati ya Magogoni na
Kigamboni Jijini Dar es salaam na kuongeza idadi ya vivuko katika eneo hilo
kufikia vitatu.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni