Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), imesaini mkataba wa upanuzi
na uongezaji wa kina cha bandari utakaowezesha bandari ya Dar es Salaam kupokea
meli kubwa za mizigo na kushindana na bandari nyingine katika pwani ya bahari
ya hindi.
Upanuzi huo
utakaofanywa na kampuni ya China Harbor Construction ya China utagharimu kiasi cha shilingi
bilioni 336 na utadumu kwa miezi 36, ambapo utahusisha uongezaji wa kina cha lango la
bandari na uongezaji wa kina cha maji kati ya gati namba 0, 1 hadi 7.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hatua hiyo
inalenga kuifufua upya bandari ya Dar es Salaam ili ifanye kazi kwa ushindani
na kuhudumia wateja wengi kuliko ilivyo sasa.
“Kukamilika kwa upanuzi na uongezaji wa kina cha maji katika gati namba 1 hadi 7 kutoka mita 8 hadi
15 kutawezesha meli kubwa na za kisasa zenye uwezo wa kubeba hadi
makontena elfu kumi na tisa kutia nanga
katika bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa
Tanzania”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa pamoja na upanuzi wa
bandari ya Dar es Salaam Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu wezeshi
ya reli na barabara ili kuhakikisha mizigo haikai muda mrefu bandarini.
“Ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge toka Dare s Salaam
hadi Kanda ya Ziwa na Kigoma na ufufuaji wa reli ya Tazara kutawezesha bandari
ya Dar es Salaam kufanya kazi kwa ufanisi na kuvutia wafanyabiashara wengi
hivyo nawataka wafanyakazi wote wa bandari
kufanyakazi kwa bidii na uadilifu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko amesema
kiasi cha dola za Marekani milioni 421, kitapatikana kwaajili ya ujenzi huo
ambapo kati ya fedha hizo Benki ya Dunia
itatoa mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 345.
Kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa adha ya baadhi ya meli
kusubiri kwa muda mrefu kupata nafasi ya kutia nanga na kutaongeza hadhi ya
bandari ya Dar es salaam na kuvutia wasafirishaji wengi kutoka ndani na nje ya
nchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni