Jumatatu, 28 Novemba 2016

ENG. NGONYANI AZINDUA SAFARI ZA NDEGE YA ATCL KIGOMA

Mkuu wa Bandari ya Kigoma Bw. Athuman Mwaibamba akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani alipoitembelea bandari ya Kigoma kukagua utendaji kazi wa bandari hiyo.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo kwa wafanyakazi wanaopakia na kushusha mizigo katika bandari ya Kigoma.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akisikiliza changamoto zinazowakabili abiria wanaotumia treni ya reli ya kati katika stesheni ya Kigoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akipata ufafanuzi kutoka kwa Kaimu mkuu wa Shirika la Posta Mkoa wa Kigoma Bw.Juma Kaungenge wakati alipokagua huduma za posta katika mkoa huo.Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa viongozi wa uwanja wa ndege na Mamlaka ya anga Mkoani Kigoma namna ya kuhudumia ndege ili kuvutia idadi ya abiria.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akiwaaga viongozi na watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  Mkoani Kigoma mara baada ya kuzindua safari za ndege Bombadier Q400 toka Kigoma kwenda Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewataka wakazi wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa kuwekeza katika biashara na vivutio vya utalii ili kunufaika na fursa ya ujio wa Ndege mpya za Shirika la ndege Tanzania (ATCL) katika kanda hiyo.

Akizungumza wakati wa kuzindua usafiri wa ndege ya ATCL kutoka Kigoma kwenda Dar es salaam Eng.Ngonyani amesema Serikali itahakikisha inaufufua ukanda wa magharibi mwa Tanzania kwa kuimarisha barabara za lami na kuwa na safari za ndege za uhakika ili kuvutia watalii kutembelea vivutio hivyo na hivyo kukuza uchumi wa mikoa hiyo.

“Kwa kuanza ATCL itakuwa na safari nne kwa wiki kuja Kigoma na idadi ya abiria ikiwa ya kutosha tutaziongeza ili kuwawezesha wasafiri na wadau wengine wa utalii kufika Kigoma kwa urahisi”, Amesema Eng. Ngonyani.

Amewataka wafanyakazi wa ATCL na viwanja vya ndege nchini (TAA), kuwa wabunifu ili kuvutia abiria wengi na hivyo juhudi za Serikali za kuiunganisha nchi kwa usafiri wa  anga zifanikiwe katika muda mfupi.

“Serikali tutaendelea kuongeza ukubwa wa uwanja wa ndege wa Kigoma na Mpanda na kutoza gharama nafuu ili kuwezesha ndege nyingi kutua katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na kuwezesha abiria na watalii wengi kunufaika na usafiri wa anga,”. Amesisitiza  Eng. Ngonyani.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ngonyani amemuagiza Mkuu wa Stesheni ya reli Kigoma Bw. Ally Shamte na Mkuu wa Bandari ya Kigoma Bw. Athumani Mwaibamba kutengeneza mkakati wa pamoja utakaowezesha bandari ya Kigoma kupata mizigo mingi kutoka katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi na hivyo kuwezesha biashara ya uhakika kufanyika katika bandari hiyo.

“Angalieni soko lilivyo na jinsi  soko linavyobadilika, hakikisheni mnaongeza wateja na kuongeza ubunifu ili watu wavutike kutumia bandari yetu”. Amesisitiza Eng. Ngonyani.
Naibu Waziri huyo amesema Serikali itaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya reli na bandari hivyo kazi ya watendaji iwe ubunifu wa kibiashara ili kuiwezesha Serikali kupata faida.

Mwenyekiti wa taasisi zilizo chini ya wizara ya ujenzi,uchukuzi na mawasiliano ambae pia ni Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Kigoma (TANROADS) eng. Narcis Choma amemhakikishi Naibu Waziri Ngonyani kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya mkoa wa Kigoma 


Alhamisi, 24 Novemba 2016

TEMESA YATAKIWA KUHARIKISHA MIFUMO YA KIELETRONIKI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Dkt. Mussa Mgwatu akieleza utendaji kazi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea Wakala huo, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), alipokagua karakana ya Wakala huo, jijini Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiteta na mmoja wa madereva wa Serikali katika karakana ya TEMESA, alipokagua karakana ya Wakala huo, jijini Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Dkt. Mussa Mgwatu akisisitiza jambo wakati  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea Wakala huo, jijini Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisisitiza jambo wakati akiongea na wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Kanda ya Dar es Salaam na Pwani (hawapo pichani) alipokutana nao jijini Dar es Salaam.

Wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) alipokutana nao jijini Dar es Salaam kuwaeleza mikakati ya Serikali kwa Wakala huo.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kuharakisha zoezi la uwekaji wa mifumo madhubuti ya kieletroniki katika vituo vyake ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Hayo ameyasema wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Wakala huo wa kanda ya Dar es Salaam na Kibaha ambapo amesema mifumo hiyo ikikamilika itadhibiti na kuongeza mapato kwa uharaka.

"Kamilisheni haraka hiyo mifumo ili kuweza kuboresha utendaji kazi wenu na wateja waweze kufurahia huduma ya uhakika na haraka", amesema Prof. Mbarawa.

Aidha ameongeza kuwa Wakala unatakiwa kupunguza idadi ya wafanyakazi wasio na tija na kuajiri wafanyakazi wachache wenye sifa kulingana na mahitaji halisi yanayohitajika katika vituo vyao.

“Msilete watumishi kwa sababu mnawajua, chukueni watu mnaowahitaji kulingana na kazi zenu ili muweze kuifanya TEMESA iwe na hadhi inayostahili”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Kwa upande wa ongezeko la gharama za vipuri vya magari zisizoendana na bei ya soko na kupelekea kupunguza wateja kwa Wakala huo, Prof. Mbarawa ameuagiza uongozi kuwaondoa wasambazaji wote wanaoongeza gharama hizo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Dkt Mussa Mgwatu amesema Wakala huo utaanza kutumia mfumo wa kitehama kwa ajili ya kutunza taarifa za matengenezo ya magari na utafanywa kwa awamu ukianzia karakana ya Dar es Salaam na Kibaha.

Dkt. Mgwatu ameongeza kuwa Mfumo huo utaweza kufatilia mwenendo wa gari na kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu (sms) kwa wateja kuwakumbusha siku za matengenezo ya magari, wateja kujua mwenendo wa matengenezo na Wakala kutambua madeni yaliyoko kwa wateja.

Katika kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuunda muundo mpya ambao utabainisha majukumu ya kila kada kwa uwazi ili kusaidia kutoingiliana kazi.