Mkuu wa Mkoa wa Mbeya
Bw. Amosi Makalla akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani walipokutana kutathimini ziara ya Naibu Waziri
huyo mkoani Mbeya.
Viongozi na wafanyakazi
wa taasisi za Serikali wametakiwa kubadilika kimtazamo ili kwenda sambamba na
malengo na matarajio ya Serikali ya awamu ya tano katika kukuza uchumi wa
viwanda na kuongeza ajira.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema Serikali
imedhamiria kufufua na kuyawezesha mashirika yake yote kufanya biashara na
kuzalisha faida ili kujitegemea na kuachana na utegemezi wa ruzuku toka
Serikalini.
Akizungumza katika
majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Mbeya Eng. Ngonyani amezitaka
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Shirika la Reli la Tanzania na Zambia
(TAZARA), na Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kubuni vyanzo vya
mapato.
“Fanyeni kazi kwa
ubunifu ili mzalishe faida na kuwa na uwezo wa kujiongezea mishahara na stahili
mbalimbali, acheni kulalamika na kutegemea ruzuku ya Serikali katika kila
jambo”. Amesisitiza Eng. Ngonyani.
Amewataka TAA
kuhakikisha ndege nyingi zinautumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe
kwani ukitumika vizuri unaweza kuwa kitovu cha uchumi kwa ukanda wa kusini na
nchi jirani kutokana na ubora wake.
Naibu Waziri huyo
amezungumzia umuhimu wa TAZARA kutafuta soko la ndani badala ya kutegemea soko
la nje pekee kwani kufanya hivyo kutapunguza mizigo mingi inayosafirishwa kwa
njia ya barabara na kuhamia kwenye reli hali itakayopunguza msongamano na
uharibifu wa barabara.
Ameziagiza taasisi
zilizo chini ya Wizara ya ujenzi kuiamini TEMESA, kufanya kazi na taasisi hiyo na
kulipa madeni zinazodaiwa ili kuiwezesha kukua na kuaminika kwa taasisi
nyingine na sekta binafsi.
Akizungumza kwa niaba
ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mwenyekiti wa
taasisi hizo Eng. Paul Lyakurwa amesema taasisi hizo zimejipanga kuboresha
miundombinu ya reli, barabara na mawasiliano ya simu na anga ili kufungua mikoa ya nyanda za juu kusini na
sehemu nyinginze za nchi na hivyo kuwezesha usafirishaji wa mazao na bidhaa
zilinazozalishwa katika mikoa hiyo kufika sokoni kwa wakati.
Naibu Waziri Ngonyani
amekuwa katika ziara ya siku tatu Mkoani Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine
amekagua meli mbili za mizigo zinazojengwa katika Ziwa Nyasa, miradi ya
barabara katika Wilaya ya Kyela, Busokelo na Rungwe na kukagua uwanja wa ndege
wa kimataifa wa Songwe na Karakana ya kutengeneza vichwa vya treni ya TAZARA.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni