Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), alipokagua karakana ya Wakala huo, jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiteta na mmoja wa madereva wa Serikali katika karakana ya TEMESA, alipokagua karakana ya Wakala huo, jijini Dar es Salaam |
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi
wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kuharakisha zoezi la uwekaji wa
mifumo madhubuti ya kieletroniki katika vituo vyake ili kuongeza ufanisi katika
utendaji kazi.
Hayo
ameyasema wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Wakala huo wa kanda ya
Dar es Salaam na Kibaha ambapo amesema mifumo hiyo ikikamilika itadhibiti
na kuongeza mapato kwa uharaka.
"Kamilisheni
haraka hiyo mifumo ili kuweza kuboresha utendaji kazi wenu na wateja waweze
kufurahia huduma ya uhakika na haraka", amesema Prof. Mbarawa.
Aidha
ameongeza kuwa Wakala unatakiwa kupunguza idadi ya wafanyakazi wasio na tija na
kuajiri wafanyakazi wachache wenye sifa kulingana na mahitaji halisi
yanayohitajika katika vituo vyao.
“Msilete
watumishi kwa sababu mnawajua, chukueni watu mnaowahitaji kulingana na kazi
zenu ili muweze kuifanya TEMESA iwe na hadhi inayostahili”, amesisitiza Prof.
Mbarawa.
Kwa
upande wa ongezeko la gharama za vipuri vya magari zisizoendana na bei ya soko
na kupelekea kupunguza wateja kwa Wakala huo, Prof. Mbarawa ameuagiza uongozi kuwaondoa
wasambazaji wote wanaoongeza gharama hizo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Naye
Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Dkt Mussa Mgwatu amesema Wakala huo utaanza kutumia
mfumo wa kitehama kwa ajili ya kutunza taarifa za matengenezo ya magari na
utafanywa kwa awamu ukianzia karakana ya Dar es Salaam na Kibaha.
Dkt.
Mgwatu ameongeza kuwa Mfumo huo utaweza kufatilia mwenendo wa gari na kutuma
ujumbe mfupi kwa njia ya simu (sms) kwa wateja kuwakumbusha siku za matengenezo
ya magari, wateja kujua mwenendo wa matengenezo na Wakala kutambua madeni
yaliyoko kwa wateja.
Katika
kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi amemuhakikishia Waziri Prof.
Mbarawa kuunda muundo mpya ambao utabainisha majukumu ya kila kada kwa uwazi
ili kusaidia kutoingiliana kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni