Jumamosi, 25 Machi 2017

SERIKALI YAONYA WAVAMIZI WA MIUNDOMBINU

Serikali imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya kukagua barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.

"Najua bado kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria", amesema Profesa Mbarawa.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzingatia viwango na  kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo hicho ili kiweze kufikia hatua ya kujenga barabara nchini.

Aidha, amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda na kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Eng. Mushubira Kamuhabwa, amesema kuwa kazi inaendelea vizuri kwani mpaka sasa mradi huo umefika asilimia 98 ambapo kazi iliyobaki ni uwekaji wa alama za barabarani.

Eng. Kamuhabwa ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria kutokana na barabara hiyo kuwa kiungo kati ya Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyaka hadi Bugene umejengwa na kampuni ya CHICO kutoka nchini China na kugharimu kiasi cha shilingi  bilioni 64.96.

Katika hatua nyengine Waziri Mbarawa ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa shule ya  Sekondari ya wavulana ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita. 

Akiwa katika shule hiyo Profesa Mbarawa ameridhishwa na kasi ya mkandarasi anayejenga shule hiyo na kusema nia ya Serikali ni kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya juu ili kukabiliana na majanga mbalimbali. 

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake na kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya juu. 

Ni takribani miezi sita tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera na kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, madaraja, hospitali, shule pamoja na makazi ya watu.

Kutokana na uharibifu huo Serikali pamoja na wadau mbalimbali ilianza juhudi za  ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo.

WAZIRI MBARAWA AKAGUA MIUNDOMBINU BUKOBA MKOANI KAGERA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), akioneshwa taarifa ya mapato na Meneja wa Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), mkoa wa Kagera, Bw. Salum Mbaya, wakati alipotembelea ofisini hapo leo.

Fundi Mitambo kutoka Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), Eng. Godfrey Mbise, akimpa maelezo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), kuhusu mfumo wa utoaji huduma katika mkongo wa taifa mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa uongozi wa Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), mkoa wa Kagera, leo, mara baada ya kukagua mitambo na mifumo iliyopo ofisini hapo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akishuka katika ndege ya Kampuni ya Ndege Nchini (ATCL), katika uwanja wa ndege wa Bukoba, mkoani Kagera alipowasili kwa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), mkoa wa Kagera Bi. Dorice Uhagile, wakati alipowasili Uwanja wa Ndege wa Bukoba ambapo amekagua uwanja huo na kuangalia changamoto mbalimbali zinazokabili uwanja huo.

Meneja wa Shirika la Posta Nchini, mkoa wa Kagera Bi. Mary Nsangila, akitoa taarifa ya utendaji kazi wa shirika hilo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa mara baada ya kukagua  maendeleo ya Shirika hilo mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kulia mbele) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), mkoa wa Kagera Eng. Zephrine Bahyona (wa pili kushoto mbele), wakati alipokuwa akikagua karakana yao na kuona changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.

TTCL KUZALISHA DOLA MIL 50.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  Profesa Makame Mbarawa ameipa miezi miwili  Kampuni ya Simu Tanzania  (TTCL), kuhakikisha kuwa inapata Dola za Kimarekani milioni 50 ili kuongeza pato kwa Kampuni na Taifa kwa ujumla kupitia Mkongo wa Taifa.

Akitoa agizo hilo leo, wilayani Bukoba mkoani Kagera, Waziri Prof. Mbarawa amesema agizo hilo limetokana na Serikali kuongeza masafa kwa kampuni hiyo kutoka 10 hadi 200 (MHZ) ambayo yana uwezo wa kuunganisha wateja wengi na wakubwa zaidi.

Amesisitiza makampuni ya Simu nchini kuchangamkia fursa ili kupata masafa yenye uwezo mkubwa kupitia mkongo huo.

"Hakikisheni mnajipanga kuipata hiyo fedha ndani ya miezi miwili na kuwapatia masafa ya kutosha wateja mlionao ndani na nje ya nchi na kujitahidi kuongeza wateja wengi zaidi", amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, ameitaka TTCL kusogeza  wigo wa kuwasiliana na wateja wakubwa ili kuwashawishi kununua masafa hayo  kulingana na mahitaji yao na hivyo kutanua wigo wa kibiashara  na kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida zaidi.

Kwa upande wake Meneja wa TTCL mkoa wa Kagera Bw. Salum Mbaya amemhakikishia Waziri huyo kuwa wataanza mara moja kazi ya kutembelea wateja wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwapatia taarifa za ongezeko la uwezo wa mkongo na kuwashiwishi kujiunga ili kupatiwa masafa wanayohitaji.

Bw. Mbaya ametaja kuwa mpaka kufikia sasa nchi zilizounganishwa na mkongo wa Taifa  ni Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Kenya na Malawi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ametembelea uwanja wa ndege wa Bukoba na kuahidi kutatua changamoto zinazoukabili uwanja wa ndege wa Bukoba ikiwemo kujenga jengo la kuongezea ndege (Control Tower) ili kuongeza ufanisi na usalama katika usafiri wa anga.

Naye, Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini mkoa wa Kagera, Bi. Dorice Uhagile, licha ya kuelezea mafanikio mbalimbali kama vile ongezeko la ndege na wateja uwanjani hapo pia amefafanua changamoto mbalimbali zinazoukabili uwanja huo na kuiomba serikali iweze kuwatatulia.

Waziri Mbarawa ameanza ziara ya kikazi wilayani Bukoba, mkoani Kagera ambapo ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.