Jumanne, 15 Novemba 2016

UJENZI WA GATI LA NYAMISATI KUANZA MWAKANI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.Edwin Ngonyani (wa kwanza kushoto) akitoa maelekezo kwa kaimu Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS)  Mkoa wa Mtwara Eng. Dotto Chacha alipokagua barabara ya Mangaka-Mtambaswala na Mangaka –Tunduru.

Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS)  Mkoa wa Mtwara Eng. Dotto Chacha akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.Edwin Ngonyani (katikati) eneo la mzunguko wa Mangaka linalohitaji marekebisho katika  barabara ya  Mangaka –Mtambaswala na Mangaka –Tunduru ambao ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.

Muonekano wa barabara ya Mangaka-Mtambaswala inayounganisha Tanzania na Msumbiji ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika barabara hii  inatarajiwa kuchochea uchumi wa mkoa wa Mtwara

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewahakikishia wananchi wa Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mafia kuwa ujenzi wa gati la kisasa katika eneo la Nyamisati utaanza wakati wowote baadaye mwakani na kukamilika ifikapo Machi 2018.

Akizungumza mara baada ya kukagua eneo litakapojengwa gati hilo katika pwani ya Nyamisati wilayani Kibiti Eng.Ngonyani amewataka viongozi na wananchi wa wilaya hizo kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu.

“Endeleeni kutunza mazingira ya eneo hili na kutunza mazingira ya bahari ili kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi katika eneo lenu, Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto inayowakabili sasa hivyo toeni ushirikiano unaohitajika ili kuiwezesha Mamlaka ya Bandari nchini(TPA) kutekeleza ujenzi wa gati hili”. Amesisitiza Eng. Ngonyani.

Naye Mbunge wa Mafia Mhe. Mbaraka Dau amemhakikishia Naibu Waziri Ngonyani kuwa kukamilika kwa gati la kisasa katika pwani ya Nyamisati kutahuisha shughuli za kiuchumi kwa wakazi  wa Mafia na Mkoa wa pwani kwa ujumla.

“Kukamilika kwa gati hili kutavutia wasafirishaji wengine kuleta vyombo vya usafiri na hivyo kushusha gharama za usafiri kati ya Kibiti na Mafia ambapo sasa ni zaidi ya shilingi elfu kumi na tatu kwa safari”. Amesema Mhe. Dau.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ngonyani amekagua barabara ya Ikwiriri-Lindi, Nanyumbu –Masugulu-Mtambaswala na Mangaka -Tunduru na kumtaka Meneja wa Wakala wa barabara Mkoa wa Mtwara Eng.Dotto Chacha kuhakikisha barabara inakuwa salama wakati wote kwa kudhibiti madereva wanaoegesha magari barabarani isivyostahili.


Naibu Waziri Ngonyani yupo katika ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Bandari na Mawasiliano katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni