Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akiwa katika picha ya pamoja na
wadau wa maendeleo alipofungua mkutano Mkutano wa 10 wa Mashauriano wa Sekta ya Uchukuzi, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa Sekta binafsi
kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika uwekezaji wa ujenzi wa miradi ya
usafirishaji nchini.
Aidha amewataka wadau
hao kuendelea kufadhili utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo chini ya sekta
hiyo ili kuchochea fursa za maendeleo.
Hayo ameyasema wakati
akifungua mkutano wa 10 wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Uchukuzi na
usafirishaji uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Michango ya Sekta binafsi
inahitajika kwa kiasi kikubwa pamoja na Serikali kuendelea kutenga fedha za
utekelezaji wa miradi ya maendeleo”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema
kuwa mafanikio ya malengo ya mwaka jana ya mkutano huo yamepelekea Serikali
kupitia sekta hiyo kuboresha usafiri wa anga kwa kununua ndege mbili za
Bombadier Q400 mwaka huu.
Ameongeza kuwa kwa
sasa Serikali ipo katika hatua za awali za ununuzi wa ndege nyingine tatu
ambazo ndege ya kwanza itawasili Mwezi Julai mwakani na nyingine mbili
zitawasili mwezi Mei na Septemba 2018.
“Mapitio ya mkutano wa
9 ni matunda ya upatikanaji wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hivyo
mikutano kama hii ina tija kwani inaisaidia kuboresha hali ya miundombinu
nchini”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.
Amesisitiza wadau
kutumia mkutano huo kama chachu ya kupata maoni na mawazo mapya ambayo
yatasaidia katika kufanikisha uboreshaji wa Sera, Sheria na kanuni za sekta ya usafarishaji nchini.
“Tumieni mkutano huu
kujadili na kushauriana ili kupata majawabu yatakayosaidia kutatua changamoto
zilizopo katika Sekta hii”, amesema Prof. Mbarawa.
Naye, Mwakilishi Mkazi
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bi. Tonia Kandiero ameipongeza Serikali
ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika uboreshaji
na ukuzaji wa Sekta ya Usafirishaji ambayo ni kiungo kikubwa katika kukuza pato
la Taifa.
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho amesema
kuwa anaimani mkutano huo utasaidia kutatua changamoto za miradi mbalimbali
iliyokuwa ikisuasua katika Sekta yake.
Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga amesema kuwa sekta yake
imefanikiwa kuunganisha kwa kiwango cha lami barabara zote ndani ya mikoa na
nchi jirani ambapo kwa sasa sehemu iliyobaki ni kuunganisha ukanda wa Magharibi.
Amezitaja barabara
ambazo zipo katika ukanda huo kuwa ni Manyoni-Tabora-kigoma,
Kigoma-Kidahwe-Kasulu, Kibondo-Nyakanazi, Sumbawanga-Mpanda-Uvinza-Kasulu,
Tabora-Koga-Mpanda, Mbeya-Chunya-Makongorosi-Rungwe na Itigi mpaka Mkiwa.
Mkutano huo wa siku
moja umewashirikisha wadau wa Sekta ya Uchukuzi na wafadhili mbalimbali katika
kujadili miradi na utekelezaji wake pamoja na kutafuta suluhu za changamoto
zinazoikabili sekta.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni