Mafundi wanaojenga
barabara ya Mafinga-Igawa sehemu ya
Mafinga –Nyigo KM 74.1 Mkoani Iringa wakiendelea na ujenzi wa karavati kubwa katika
eneo chepechepe maarufu Majinja wilayani Mufindi.
|
Muonekano wa Mtambo wa
kusaga kokoto pamoja na shehena ya kokoto zinazotumika katika ujenzi wa
barabara ya Mafinga –Igawa.
|
Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amemtaka mkandarasi China Civil Engeneer
Construction Cooporation (CCECC), anayejenga barabara ya Mafinga-Nyigo km 74.1
na (CRSG) anayejenga sehemu ya Nyigo –Igawa KM 63.8 kuongeza kasi ya ujenzi ili upanuzi na
uimarishaji wa barabara hiyo ukamilike kwa wakati.
Akizungumza mara baada
ya kukagua ujenzi huo Eng. Ngonyani amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS)
Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole kuhakikisha upana wa barabara hiyo na ubora
wake unakidhi malengo ya Serikali ili barabara hiyo ili idumu kwa muda mrefu na
kupunguza msongamano na ajali zinazoepukika.
“Barabara hii ambayo
ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM inaunganisha bandari ya Dar es Salaam na
nchi za Zambia na Malawi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hivyo ni lazima
isimamiwe kikamilifu ili idumu kwa muda mrefu”, amesisitiza Eng. Ngonyani.
Akitoa taarifa ya
ujenzi wa barabara hiyo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole
amesema tayari kilomita 18 kati ya 74.1 katika sehemu ya kwanza ya Mafinga
–Nyigo imeshawekwa lami na Mkandarasi ameunda
timu tatu ili kuharakisha ujenzi huo.
“Ujenzi wa barabara ya
Mafinga -Igawa unahusisha mikoa mitatu ambapo Kilomita 74.1 ziko katika mkoa wa
Iringa Mafinga-Nyigo, Kilomita 52 ziko katika mkoa wa Njombe Nyigo-Halali na
Kilomita 12 ziko katika Mkoa wa Mbeya Halali-Igawa hivyo mimi pamoja na
wenzangu tumejipanga kuhakikisha barabara hii inakamilika Novemba mwakani kama
ilivyopangwa”, amesisitiza Eng. Kindole.
Naye Meneja Mradi wa
ujenzi wa barabara hiyo Sehemu ya Mafinga – Nyigo KM 74.1 Richard Guo amemhakikishia
Naibu Waziri huyo kwamba kasi yao ya ujenzi ni nzuri na barabara hiyo
imeimarishwa ili kukidhi mahitaji na itakamilika kwa wakati.
Zaidi ya shilingi
bilioni 116 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya
kwanza yaani Mafinga- Nyigo km 74.1 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya
Tanzania na Benki ya Dunia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni