Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na wananchi mara baada ya kumaliza kukagua daraja la
waenda kwa miguu lililopo eneo la Buguruni Jijini Dar es salaam.
|
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Kampuni ya Mkandarasi
ya Sumitomo Mitsui inayojenga mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika
makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara kumaliza ujenzi huo kwa
wakati ili kusaidia kupunguza tatizo la msongamano.
Akizungumza mara baada
kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jijini Dar es salaam, Profesa Mbarawa
amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutajenga historia nchini kutokana na kuwa ni wa mwanzo kujengwa.
“Nimefurahi kuona
mradi huu upo katika hatua nzuri, naomba mhakikishe mradi huu unakamilika kwa
ubora na kwa wakati ili tatizo la msongamano lililopo katika maeneo haya
kupungua au kuisha kabisa”, amesema Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa
amemtaka Mkandarasi kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa umakini na kwa uangalifu wakati wa kipindi
chote cha ujenzi ili kutokusababisha foleni katika eneo hilo.
Aidha, Waziri Mbarawa amewataka
wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi huyo ili kurahisisha
kazi za ujenzi huo kukamilika kwa wakati na kupata matokeo chanya.
“Nawaomba watanzania
wenzangu kuwa wavumilivu na usumbufu wowote utakaojitokeza katika kipindi hiki chote,
kwani ukamilifu wa mradi huu utasaidia kupunguza tatizo la msongamano katika
barabara hizi”, amefafanua Waziri Mbarawa.
Katika hatua nyingine,
Profesa Mbarawa amekagua daraja la watembea kwa miguu eneo la Buguruni Sheli na
kuwataka wananchi wa maeneo hayo kulitunza daraja hilo ambalo uwepo wake umesaidia
kupunguza ajali katika maeneo hayo.
“Ni matumaini yangu
sasa wakazi wa maeneo haya mtavuka kwa
amani kupitia daraja hili, na ajali zilizokuwa zikitokea maramara hazitakuwepo
tena”’, amesema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake,
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Patrick Mfugale
amemuahidi Waziri huyo kumaliza kwa wakati ujenzi huo na kumhaakikishia Waziri
kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakuwa na viwango vilivyo bora.
Mradi wa Tazara
Flyover ni msaada kutoka Serikali ya Japan ambao umegharimu shilingi bilioni
93.4 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2018.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni