Serikali
imesema itaongeza mabehewa ya abiria na mizigo katika Shirika la Reli la
Tanzania (TRL), kwa lengo la kutatua adha ya usafirishaji kwa watumiaji wa
reli ya kati katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.
Akizungumza
katika ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa uhaba wa mabehewa ya abiria
umesababisha wananchi wa maeneo hayo
kutumia njia zisizo rasmi za ununuzi wa tiketi kwa ajili ya usafiri huo.
"Serikali
imetambua changamoto kubwa ya usafiri inayowakabili wakazi wa mikoa hii, hivyo
ni wakati muafaka kwa TRL kuongeza mabehewa matatu ili kupunguza adha ya
usafiri", amesema Prof. Mbarawa.
Aidha,
Waziri Prof. Mbarawa ameupongeza uongozi wa TRL kwa kuokoa matumizi ya zaidi ya
Shilingi milioni 100 kwa kukarabati mabehewa ya mizigo 23 kwa kutumia wataalam
wazawa wa shirika hilo.
Ameongeza
kuwa Shirika hilo limetekeleza dhana ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza
matumizi ya fedha na kuzingatia thamani ya fedha na kazi inayofanyika.
“Nawapongeza
kwa kazi nzuri mnayofanya ya kupunguza matumizi ya fedha mnazopata kwenye
Shirika, ninaomba muendelee kutumia vyanzo vya ndani ili shirika lifikie hatua
ya kujitegemea” amesema Profesa Mbarawa.
Naye,
Meneja wa Usafirishaji wa TRL, mkoa wa Tabora Fredrick Masangwa ameiomba
Serikali kuendelea na maboresho katika miundombinu ya reli kwa kiwango sawa na
jinsi inavyoboresha miundombinu shindani ya barabara ili kuwepo na ushindani
sawa katika sekta hizo mbili za usafirishaji.
Katika
hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya
Ndono-Urambo kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 52 na barabara ya
Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi na
ukarabati wake.
Profesa
Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo iende sambamba na viwango bora
vya ujenzi wa barabara vilivyomo kwenye mikataba iliyosainiwa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abeli Busalama ameipongeza Serikali
kwa juhudi za ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika wilaya
hiyo kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza fursa za kiuchumi katika
wilaya yake na wilaya za jirani pamoja na mikoa inayozunguka wilaya hiyo.
Mbunge
wa Jimbo la Kaliua Mhe. Magdalena Sakaya amemuomba Waziri huyo kufikisha
mawasiliano ya simu kwenye wilaya hiyo hususan vijijini ili kuweza kurahisisha mawasiliano
kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Waziri
Mbarawa amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili katika Mkoa wa Tabora ambapo
amekagua miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, reli na mawasiliano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni