Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva wote wa malori ya mchanga na kokoto watakaobainika kutofuata sheria za ubebaji wa bidhaa hiyo na hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma
katika ziara yake ya kukagua barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa
kilometa 50 ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali inatumia fedha
nyingi kujenga miundombinu ya barabara kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa
ujumla hivyo haita mvumilia mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombu hiyo
kwa makusudi.
“Kuanzia
sasa Serikali haitavumilia madereva wasiozingatia kanuni na sheria za
usafirishaji wa mizigo katika barabara nchini, hivyo nawaagiza Mameneja wa
TANROADS katika mikoa yote nchini kusimamia sheria ili kudhibiti miundombinu ya
barabara, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ameliomba Jeshi la Polisi
kushirikiana vema na makandarasi wanaojenga miundombinu ya barabara katika
maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya
watu wasio waaminifu ambao wanaiba vifaa vya makandarasi jambo linalochangia kukwamisha
shughuli za ujenzi wa barabara.
Amewataka wananchi wa Wilaya ya Kasulu
kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau
Group Corporation anayejenga barabara hiyo ili kuwezesha ujenzi huo kukamilika
haraka.
Naye
Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma, amebainisha changamoto
zinazokabili mradi huo kuwa ni wizi wa mafuta na vifaa vya ujenzi hali
inayosababisha mradi kusuasua.
"Wananachi
tambueni kuwa fedha hizi ni za kwenu mnapohujumu vifaa vya ujenzi ni dhahiri
mnajicheleweshea maendeleo na kukwamisha fursa za kiuchumi katika wilaya
yenu", amesema Eng. Choma.
Kwa upande wake
Mhandisi Mkazi Mekbib Tesfaye anayesimamia mradi huo kutoka Kampuni ya DOCH
Limited, amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 24 ambapo kwa sasa kazi
inayofanyika ni ujenzi wa madaraja mawili na makalvati katika barabara hiyo.
Katika hatua
nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ametembelea Chuo cha Mamlaka ya Hali ya Hewa
Mkoani Kigoma na kuahidi uongozi kuwa atazishughulikia haraka changamoto kadhaa zinazokikabili chuo
hicho ili kuweka mazingira rafiki ya kujisomea kwa wanafunzi wanaosomea
taalauma hiyo.
“Nitahakikisha
chuo hiki kinajengewa mabweni ya wanafunzi pamoja na kuongeza gari kwa ajili ya
shughuli mbalimbali zinazofanyika hapa”, amefafanua Waziri Mbarawa.
Kaimu Mkuu wa
Chuo hicho Peter Mlonganile wakati akisoma
taaraifa ya chuo hicho kwa Waziri huyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na
changamoto hizo chuo hicho kinaendelea
kutoa mafunzo hayo kwa viwango vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuzitatua changamoto ndogo
ndogo zinazo kikabili chuo hicho.
Prof. Mbarawa
yuko katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege,
katika mkoa wa Kigoma ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu
hiyo na kuuwezesha mkoa kufanya biashara kirahisi na mikoa mingine ya Tanzania
na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni