Mwenyekiti wa Bodi ya
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Prof. Ninatubu Lema, akifafanua jambo kwa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto),
wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo. Kulia kwake ni MKurugenzi wa Miundombinu ya
Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Hussein Mativila.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Bodi mpya ya Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kusimamia Menejimenti ya Mamlaka hiyo
katika Idara ya Utawala na Rasilimali watu ili kuhakikisha ajira zote zinazotolewa zinazingatia sifa na vigezo
vya kuajiri.
Akizungumza katika
uzinduzi wa Bodi hiyo mpya jijini Dar es salaam pamoja na mambo mengine,
Profesa Mbarawa ameisisitiza bodi hiyo kuifanyia kazi Ripoti ya Uchunguzi wa
uendeshaji wa Viwanja hivyo nchini na kufanya mabadiliko mara moja.
“Nataka muipitie
ripoti niliyomkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mkuu na mufanyie maamuzi, suala la
kuajiri watu kiholela, ninataka wote waliandikwa kwenye ripoti hiyo kuwa hawana
sifa watolewe wapishwe watu wenye sifa ili waweze kufanya kazi”, amesema Waziri
Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa
ameitaka Bodi hiyo kusimamia kwa uadilifu miundombinu yote ya viwanja vya ndege
nchini na kuhakikisha mashine za ukaguzi zinafanya kazi masaa 24 ili kudhibiti
mianya yote ya rushwa.
Ameitaka Bodi hiyo
kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato katika viwanja vyote ili kuweza kufikia
lengo lililowekwa na kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, Profesa Mbarawa
ameitaka Bodi hiyo kushirikiana na wafanyakazi wa Viwanja hivyo katika mambo
mbalimbali ili kuboresha utendaji na kuweka uwazi katika utoaji wa huduma
katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Ninatubu Lema amemhakikishia Waziri huyo kuwa
ataongeza ushirikiano na wafanyakazi wote na kusimamia maagizo yote
yaliyotolewa.
Ameahidi kuboresha
huduma katika viwanja vyote nchini na kusema kuwa umuhimu wake utaongeza mapato katika viwanja
hivyo na nchi kwa ujumla.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni