Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akimsikiliza mmoja wa
wajumbe waliohudhuria katika Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS), mkoani Dodoma.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameuagiza Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS) kuboresha Idara ya Mipango na Usanifu katika wakala
huo ili kupata matokeo mazuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
Prof. Mbarawa
ameutaka wakala huo kuboresha kanuni zinazosimamia aina ya vyombo vya moto
vinavyotumia barabara zote nchini ili kuweza kusaidia miundombinu hiyo
kudumu muda mrefu.
Akizungumza
mkoani Dodoma katika ufunguzi wa Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Wakala huo
Prof. Mbarawa amesema kuwa wakala unabidi uanze kubadili aina ya mfumo wa
usanifu uliokuwa ukitumika awali na badala yake utumike usanifu wa kisasa
unaoendana na mahitaji halisi ya watumiaji wa barabara hizo.
“Kama mnaona
kuna mabadiliko yoyote mnayohitaji kuyafanya ili barabara zetu zidumu, boresheni
kanuni na mlete kwangu ili nizifanyie kazi”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa
katika kuboresha utendaji katika wakala huo, Serikali ina mpango wa kuwapa
fursa za ajira wahandisi hususani wanawake na kuwajengea uwezo na kuweka
uwiano katika taalamu hiyo.
Aidha Waziri
Prof. Mbarawa ameahidi kuongeza fedha za uendeshaji kwa wakala huo ili
kuuwezesha kutekeleza miradi mbalimbali inayoendelea nchini.
“Kumbukeni
majukumu ya Wakala yameongezeka sasa hamtajenga barabara pekee, mmeongezewa
jukumu la kujenga miundombinu ya viwanja vya ndege hivyo ni muhimu kujipanga
kutekeleza kazi hii”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye, Mtendaji Mkuu
wa TANROADS, Eng. Patrick Mfugale ameahidi kushughulikia ujenzi wa viwanja vya
ndege ikiwemo kufanya kazi kwa weledi na uadilifu kama ambavyo wakala huo
unatekeleza miradi yake ya barabara.
Ameongeza kuwa
Wakala unaendelea kufanya kazi na Makandarasi wenye uwezo na wanaozingatia
thamani ya fedha katika miradi yote inayotekelezwa nchini.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi ya TANROADS, Eng. Hawa Mmanga amemuahidi Waziri Prof.
Mbarawa kufanya kazi kwa uadilifu, bidii, na kuzingatia thamani ya fedha katika
miradi yote inayotekelezwa na wakala.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni