Muonekano wa kivuko
kipya cha MV Kazi kikiwa katika hatua za awali za ujenzi wake. Kivuko hicho
kinatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu.
|
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akiongea na mwanafunzi Arafat
Kondo wakati alipotembelea kivuko cha MV. Kigamboni kujionea utendaji wake.
|
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akishuka kwenye pantoni mara
baada ya kukagua utendaji wa kivuko cha MV. Kigamboni.
|
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa ameuagiza uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA),
kuhakikisha wanaweka mipango madhubuti ya kuongeza mapato katika vivuko vya MV.
Kigamboni na MV. Magogoni kutoka Shilingi Milioni 14 ambazo zinakusanywa hivi
sasa hadi kufikia Milioni 19 kwa siku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua
vivuko hivyo na kuongea na Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu Prof.
Mbarawa amesema kuwa kipimo cha utendaji huo utafanyika ndani ya miezi minne ili
kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa vivuko hivyo na kuweza kufikia
malengo.
“Hatushindwi kutafuta mtu mwingine mwenye ujuzi na
utendaji wa kazi uliotukuka, kama lengo la kukusanya milioni 19 halitafikiwa basi
mkuu wa kivuko atafute kazi nyingine, na
tutafanya hivyo mpaka tuhakikishe tunapata atayeweza kukusanya kiwango hiki”,
amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameutaka Wakala huo kuboresha mifumo
ya ukusanyaji wa mapato katika vivuko hivyo na kuwa wa kieletroniki ili
kudhibiti ubadhilifu unaofanywa na watumishi wasio waaminifu wakati wa utoaji
huduma.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amejionea
maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha MV. Kazi nakusema kuwa kivuko hicho kitarahisisha
usafiri kwa wakazi wa Kigamboni.
Aidha, amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Songoro
Marine Transport kumaliza utengenezaji wa kivuko hicho ifikapo Mwezi Disemba
mwaka huu ili watanzania wapate huduma bora za usafiri.
Ameongeza kuwa Kampuni hiyo ihakikishe kuwa inasimamia
upatikanaji wa injini za Kivuko hicho kwa wakati ili kusaidia ujenzi huo kukamilika
kwa muda uliopangwa.
“Nina imani na kasi mnayokwenda nayo, na nina
uhakika Kivuko hiki kitamalizika kwa wakati naomba muwe waangalifu na
kuhakikisha kwamba injini za kivuko hiki zinawasili mapema”, amesisitiza Prof.
Mbarawa.
Naye Mkurugenzi wa Karakana ya Dar es Salaam wa
Kampuni ya Songoro Marine, Saleh Songoro amesema kuwa ujenzi wa Kivuko
cha MV Kazi upo katika hatua nzuri ambapo kwa sasa wanakamilisha kazi ya
kuchomea milango katika kivuko hicho.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mgwatu
amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa maagizo yote yatatekelezwa ikiwemo
kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Wakala huo.
Dkt. Mgwatu amewataka wananchi kuwa na subira
wakati kivuko cha MV. Kazi kinamalizika kujengwa kwani kitapunguza kama sio
kuondoa msongamano uliopo sasa katika maeneo ya Magogoni na Kigamboni.
Ujenzi wa kivuko cha MV Kazi ulianza Mwezi Juni
mwaka huu ambapo kina uwezo wa kubeba tani 170 sawa na watu 800 na magari 22
kwa wakati mmoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni