Mwakilishi wa Kibiashara
kutoka Ubalozi wa Uingereza anayesimamia nchi ya Tanzania na Kenya Bw. Lord
Hollick (wa pili kulia) akifafanua jambo
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa
kwanza kulia) wakati alipomtembelea ofisini kwake kuzungumzia masuala ya kuboresha
miundombinu nchini. Kushoto ni Balozi wa Uingereza nchini Bi Sarah Cookie.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Kampuni ya
Simu Tanzania (TTCL), kutafuta wateja wa kuhifadhi kumbukumbu zao kwenye Kituo mahiri
cha kuhifadhi kumbukumbu cha Taifa (Internet Data Center), jijini Dar es Salaam.
Waziri Prof. Mbarawa pia amemuagiza Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni hiyo kuwa mbunifu na kuanza kufuata
wateja ana kwa ana na si kusubiri wateja hao kumfuata ofisini kwake.
Prof.
Mbarawa ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kushtukiza katika jengo hilo
lililopo eneo la Kijitonyama ambapo ameelezea umuhimu wa kufanya jitihada za
haraka kutafuta wateja hao kwa lengo la kuongeza pato cha Taifa.
"Natoa
wiki mbili kwa Mkurugenzi wa Masoko kuhakikisha analeta wateja wa kuhifadhi
kumbukumbu zao katika kituo hiki, ikishindikana atupishe tutafute watu wanaofaa
katika taaluma hiyo", amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Prof.
Mbarawa amesema kuwa Kituo hicho kimeimarishwa kiusalama kwani kimeunganishwa
na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo wateja wataweza kuchukua taarifa zao
kwa uharaka zaidi.
Ameongeza
kuwa masuala yote yanayohusu makubaliano ya kibiashara katika kituo hicho yawekwe
kwa njia ya maandishi ili kuweza kuweka kumbukumbu sahihi na ufatiliaji
inapohitajika.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Mawasiliano), Eng. Peter Mwasalyanda amemuahidi
Waziri Mbarawa kutekeleza yale yote aliyoyaagiza yafanyike ili kuboresha huduma
katika kituo hicho.
Katika
hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekutana na Mwakilishi wa Kibiashara
kutoka ubalozi wa Uingereza anayesimamia nchi ya Tanzania na Kenya Bw. Lord
Hollick na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kuboresha miundombinu nchini.
Kituo mahiri cha Internet Data
Centre ni cha kwanza kujengwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na
Kati na
asilimia 75 zimetengwa kwa ajili ya kutunza
taarifa kutoka sekta binafsi na asilimia 25 itatunza taarifa za Serikali hivyo
ni fursa mpya kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali wenye taarifa nyingi
kuzihifadhi na kuzitumia wanapozihitaji.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni