Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua ramani inayonyesha
miundombinu ya barabara nchini wakati wa uzinduzi wa mkutano wa saba wa sekta
ya Miundombinu ya barabara na reli, jijini Dar es salaam.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa sekta
ya miundombinu ya Reli na Barabara kushirikiana na Serikali katika kuchangamkia
fursa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta hiyo hapa nchini.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Saba wa
wadau wa Sekta hiyo, Prof. Mbarawa amesema kwa sasa Serikali kupitia Rais wa Awamu
ya Tano inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta kutoka
Tanga hadi nchini Uganda, ujenzi wa barabara ya kulipia wa Dar es Salaam-Chalinze
KM 144 (Dar-Chalinze Express way) na
ujenzi wa reli ya kati hivyo ni muhimu kwa wadau hao kutumia mkutano huo katika
kuijadili miradi hiyo.
“Ni matumaini
yangu katika mkutano huu mtajadili kwa pamoja namna ya kushirikiana na Serikali
katika kutekeleza fursa za ujenzi wa miundombinu hapa nchini ikiwemo kuungana
na Serikali (Public Private Partnership) au
kwa njia nyingine yoyote”, amesema Waziri Mbarawa.
Aidha, Profesa
Mbarawa amewataka wadau hao kutumia mkutano huo wa siku mbili kujadili namna
bora ya kutunza na kuboresha miundombinu ya reli na barabara ili kuweza kudumu
kwa muda mrefu.
Amesisitiza
wadau hao kuja kwa wingi nchini na kuwekeza katika sekta hiyo ili kupanua
ushindani wa kibiashara katika soko la kitaifa na kimataifa.
Wazri Mbarawa
amebainisha kuwa Serikali inaendelea kutafuta pesa kutoka kwa wadau mbalimbali
na kushirikisha taasisi binafsi kupitia mpango wa kushirikiana baina ya
Serikali na Taasisi hizo (Public Private
Partnership) ili kutekeleza miradi ya miundombinu ya reli na barabara
nchini.
Kwa Upande
wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA)
Eng. Bruno Ching’andu amesema kuwa licha ya TAZARA kuwa na treni za umma
zinazotoa huduma za usafiri nchini bado inakabiliwa na changamoto nyingi
ikiwemo uhaba wa fedha katika uendeshaji wa shirika hilo ikiwemo gharama za
ujenzi na ukararabati wa mabehewa.
Mkutano huo wa
siku mbili umewakutanisha wadau wa miundombinu ya barabara na Reli kutoka
Taasisi za Serikali na wadau mbalimbali wa sekta hiyo kutoka ndani na nje ya
nchi lengo likiwa ni kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha miundombinu hiyo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni