Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto), pamoja na watendaji
wa Wizara hiyo wakishuka kutoka katika Kivuko cha Mv. Tanga mara baada ya
uzinduzi. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya
Ujenzi). Eng. Joseph Nyamhanga.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua kivuko kipya na cha
kisasa cha Mv. Tanga kinachotoa huduma ya usafirishaji kati ya Pangani na Bweni
na kuzindua Gati ya Bandari ya Pangani wilayani pangani mkoani Tanga.
Akizungumza katika
uzinduzi huo Waziri Mbarawa amesema kuwa ujio wa kivuko hicho utafungua fursa
za kibiashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi wilayani hapo.
“Naamini ujio wa
kivuko hiki utarahisisha huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi wilayani
hapa, hivyo naomba mkitunze vizuri kivuko hiki ili kiweze kudumu kwa muda
mrefu”, amesema Prof.Mbarawa.
Ameongeza kuwa katika
kuhakikisha huduma za kivuko zinakuwepo muda wote wilayani hapo, Serikali kupitia
Wizara hiyo imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa boti ambayo itatumika kama
mbadala wa usafiri wakati wa usiku katika maeneo hayo ambapo kivuko cha
Mv.Tanga hakifanyi kazi.
Kuhusu ujenzi wa Gati
ya bandari ya Pangani Waziri Mbarawa ameseama kuwa ujenzi wa gati hiyo
utapelekea Meli kubwa kuweza kutia nanga na kurahisisha usafiri wa moja kwa
moja kutoka Pangani kwenda visiwa vya Unguja na Pemba.
Amefafanua kuwa
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataanzisha huduma ya boti za
haraka kutoka Pangani kwenda Mkokotoni Zanzibar hivyo kufungua fursa za
kibiashara na kitalii baina ya Tanga na Zanzibar.
Kwa upande wa huduma
za mawasiliano ya simu wilayani hapo, Prof.Mbarawa amesema kuwa huduma hiyo
itaanza mwezi Desemba mwaka huu kwa mkandarasi kufika na kuanza ujenzi wa
miundombinu ya simu na hivyo kuondoa tatizo la mawasiliano wilayani hapo.
Katika hatua nyingine
Prof. Mbarawa ameahidi kuanza ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani-Saadani hadi
Bagamoyo (KM 242) kwa kiwango cha lami ifikapo mwakani.
Amefafanua kuwa ujenzi
wa barabara hiyo utakuwa wa awamu ili kuweza kuharakisha kukamilika kwake
ambapo awamu ya kwanza itahusisha kipande cha barabara ya Tanga- Pangani (KM 50)
na kuongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utafungua fursa za kiuchumi kati ya
Tanga na Pangani.
“Naahidi kujenga
barabara hii ambayo ni kiungo kati ya Tanga na Pangani, naamini ukamilifu wake
utalete maendeleo mkoani hapa”. Amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Eng.Joseph Nyamhanga amezipongeza kampuni za Songoro Marine
na Alpha Logistic kwa kumaliza kwa wakati ujenzi wa kivuko na Gati ya bandari
hiyo.
Naye Kaimu Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Eng.Manase Ole-kujan amesema kuwa
kivuko cha Mv.Tanga kimejengwa kwa sh.bilioni nne ambapo kina uwezo wa kubeba
tani 50 abiria 100 na magari madogo 6 kwa wakati mmoja.
Ujenzi wa Kivuko cha
Mv. Tanga ni moja ya utekelezaji wa ahadi ya Mhe.Rais Dkt.John Pombe Magufuli
aliyoitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wilayani Pangani
Mkoani Tanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni