Jumatano, 14 Septemba 2016

PROF. MBARAWA ATOA MIEZI SITA KUMALIZA UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE WA MWANZA.




Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi Nyanza Road Construction inayojenga barabara ya Furahisha hadi Pasiansi KM 2.8 wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo, jijini Mwanza.

Mkandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Construction inayojenga barabara ya Furahisha hadi Pasiansi akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo jijini Mwanza.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group anayejenga uwanja wa ndege wa Mwanza kumaliza kazi ya upanuzi wa uwanja huo ifikapo mwezi Februari Mwakani.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo alipokuwa akikagua kazi ya ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza pamoja na daraja la watembea kwa miguu lililopo maeneo ya furahisha, jijini Mwanza.

Profesa Mbarawa amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja huo kutaimarisha hali ya usafiri wa anga kwa wakazi wa Mwanza na mikoa mingine na hivyo kukuza shughuli za kibiashara nchini.

“Hakikisheni upanuzi wa uwanja wa ndege huu unakamilika haraka ili kurahisisha na kuboresha huduma za usafirishaji kiwanjani hapa”, amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Construction kumaliza kwa wakati upanuzi wa barabara ya ‘Mwanza-Airport’ eneo linaloanzia Ghana Quarters hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza KM 9.15 pamoja na daraja la watembea kwa miguu la furahisha ili kukuza uchumi na kupunguza kero ya msongamano wa magari katika jiji la Mwanza.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka wananchi wa Mwanza kutoharibu miundombinu ya barabara na madaraja ambayo Serikali inatumia gharama kubwa katika utengenezaji wake.

“Naomba muitunze na kuithamini miundombinu hii kwani Serikali inatumia gharama kubwa katika kutengeneza na kukarabati”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza ni mkakati wa Serikali kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unaboreshwa kuwa wa kisasa na wa kimataifa ili kuwezesha ndege kubwa kutua kwa wingi na kuwa kiungo muhimu kwa mikoa 10 ya kanda ya Ziwa na Kati.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni