Baadhi ya nondo zinazotumika
kutengeneza mataruma katika kiwanda cha Kongolo cha TAZARA mkoani Mbeya.
Wakati Serikali ikiwa katika hatua za kumpata
mkandarasi wa ujenzi wa reli ya kisasa nchini (Standard Gauge), Mamlaka ya reli
ya Tanzania na Zambia (TAZARA) imesema imewasilisha andiko kwa Kampuni miliki
ya rasilimali za Reli (RAHCO) ili kuanza utengenezaji wa mataruma na uzalishaji
wa kokoto zitakazotumika kwenye ujenzi wa reli hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mhandisi Mzalishaji
wa kiwanda cha kuzalisha mataruma cha TAZARA mkoani Mbeya, Eng. Boniface Phiri ikiwa
ni siku chache baada ya RAHCO kutangaza zabuni hiyo ambapo amesema kuwa kiwanda
hicho kina uwezo mkubwa wa kuzalisha mataruma kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Eng. Phiri amesema pamoja na agizo la
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alilolitoa kwa mamlaka hiyo Mwezi mmoja
uliopita alipotembelea kiwanda hicho na kuelekeza kuwa Mamlaka ijipange kuzalisha
mataruma na kokoto.
“Mamlaka imejitathmini na kuona kwamba
kutokana na uwezo tulionao tumeshawasilisha andiko letu kwa RAHCO na tunasubiri
majibu yao ili kuanza kazi ya uzalishaji”, amesema Eng. Phiri.
Amebainisha kuwa kwa sasa Mamlaka inaboresha
mitambo na kuangalia namna ya kuanza kutumia teknolojia ya mvuke kwenye uzalishaji
ili kuongeza idadi ya mataruma na ubora
unaokidhi viwango ambapo kwa siku kiwanda huzalisha mataruma zaidi ya 200.
Aidha Eng.Phiri ameishukuru Serikali Ya
Tanzania na Zambia kwa kuisadia Mamlaka hiyo tani 300 za nondo ambazo
zimesaidia kuongeza uzalishaji wa mataruma katika kiwanda.
Kwa upande wake Mhandisi Mzalishaji wa mgodi
wa kokoto Eng. Juma Mizambwa amesema uzalishaji wa mataruma unaenda sambamba na
uzalishaji wa kokoto ambapo kwa sasa mgodi huo unazalisha tani 180 kwa siku.
Mradi wa ujenzi
wa Reli ya Kisasa unatarajiwa kuanza Mwezi Desemba mwaka huu ambapo kwa mwaka wa
fedha 2016/17 Serikali imetenga shillingi Trilioni moja kwa ajili ya
utekelezaji wake.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni