Sehemu ya eneo la
kuegeshea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Arusha ambao unakabiliwa na ufinyu wa
maegesho ya ndege ambapo Serikali iko katika hatua za kuuboresha.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi M/S Hanil
Jiangsu J/V anayejenga barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1 na
barabara ya mchepuo (Arusha bypass) yenye urefu wa KM 42.4 kuhakikisha barabara
hizo zinakamilika ifikapo mwezi Machi na Oktoba mwakani.
Profesa Mbarawa
amesema hayo mara baada ya kukagua ujenzi barabara hizo na kujiridhisha na
hatua iliyofikiwa kwa barabara zote.
“Meneja hakikisha
ujenzi wa barabara hizi unakwenda sambamba na ujenzi wa sehemu ya barabara
inayoelekea Ikulu ya mjini Arusha ili kuiunganisha vizuri barabara hiyo kwa
kiwango cha lami”, amesema Prof. Mbarawa.
Amemtaka Mkuu wa
Wilaya ya Arusha Bw. Gabriel Daqarro kushirikiana na Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), mkoani humo kuhakikisha maji yanayopita kwenye madaraja yaliyopanuliwa
kufuatia ujenzi unaoendela hayasababishi mafuriko kwenye makazi ya wananchi.
Kwa upande wake Meneja
wa TANROADS mkoa wa Arusha Eng. Johnny Kalupale amemhakikishia Waziri Prof.
Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara mkoani Arusha utakamilika kwa wakati na ubora
unaotakiwa.
“Tumejipanga
kuhakikisha barabara ya Sakina-Tengeru na ile ya mchepuo zote zitakamilika kama
ilivyopangwa ili kupunguza msongamano hali itakayovutia ongezeko la watalii na
hivyo kukuza uchumi wa mkoa wa Arusha”, amesema Eng. Kalupale.
Katika hatua nyingine
Waziri Prof. Mbarawa amekagua uwanja wa ndege wa Arusha na kusisitiza kuwa nia
ya Serikali ni kuupanua uwanja huo ambao ni wa nne kwa uingizaji wa mapato
nchini ili kuondoa msongamano uliopo sasa.
“Wakati Serikali
tunajipanga kuongeza uwanja huu na nyinyi mjipange kuongeza mapato ili jitihada
za Serikali ziendane na ubunifu wa watendaji”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Meneja wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), mkoa wa Arusha Bw. Elipid Tesha amesema
uwanja huo ambao ni kitovu cha utalii katika ukanda wa Kaskazini ukiongezwa
utaruhusu ndege nyingi kutua na hivyo kuuongezea mapato ambapo kwa sasa takribani
miinuko 110 ya ndege hufanyika kila siku katika uwanja huo.
“Kwa sasa uwanja wa
ndege wa Arusha una barabara ya kurukia yenye urefu wa KM 1.6 hali
inayosababisha baadhi ya ndege kushindwa kuutumia ila mkakati wa uwanja huo ni
kuuongeza uwe na urefu wa KM 2.5”, amesisitiza Bw. Tesha.
Uwanja wa Ndege wa
Arusha uliojengwa mwaka 1956 ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za utalii
katika mkoa huo uko KM 7 kutoka Arusha Mjini na una eneo la ekari 280 na uzio unaoimarisha
usalama wakati wote.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni