Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga
akishuka kutoka katika kivuko cha Mv. Magogoni.
|
Wakazi wa Kigamboni
wakielekea kupanda kivuko cha Mv.
Magogoni mara baada ya kuanza kutoa huduma za usafiri kati ya Magogoni na Kigamboni.
|
Muonekano wa Kivuko
cha Mv. Magogoni kikiwa majini mara baada ya ukarabati wake kukamilika. |
Kivuko cha MV.
Magogoni kimepokelewa na kuanza kazi rasmi ya kutoa huduma za usafirishaji kati
ya eneo la Kigamboni na Magogoni mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wake
mkubwa.
Katika kuhakikisha
huduma za vivuko zinaimarika nchini, Serikali kupitia TEMESA inatarajia kukifungua
kivuko cha Mv Pangani II mkoani Tanga mwezi huu na kununua kivuko kingine kipya
ambacho kitatoa huduma kati ya Kigongo na Busisi mkoani Mwanza.
Akizungumza jijini Dar
es salaam mara baada ya kukipokea kivuko hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga amesema kuwa
kukamilika kwa ukarabati wa kivuko hicho kutaimarisha huduma za usafirishaji kwa
wakazi wa Kigamboni.
“Kivuko kimeanza kazi
rasmi, matumaini yangu adha ya usafiri kwa wananchi wa Kigamboni na Magogoni
itapungua”, amesema Eng. Nyamhanga.
Aidha, Katibu Mkuu
huyo amebainisha ujenzi wa kivuko kingine cha tatu kwa ajili ya kuboresha huduma ya usafiri ili
kuweza kusaidiana na vivuko vingine vinavyofanya kazi katika maeneo hayo.
Amefafanua kuwa kivuko
hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu na kitakuwa na uwezo wa
kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.
Kuhusu utoaji huduma
katika vituo vya kukatia tiketi katika maeneo hayo Eng. Nyamhanga amemuagiza
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Eng. Manase Ole
Kujan kuboresha mfumo wa kukatia tiketi kuwa wa njia ya kadi ambayo itamruhusu
mtumiaji kukata tiketi kwa kipindi anachotaka.
“Hakikisheni kuwa
mfumo uliopo sasa unabadilika na kuwa wa kadi ili kumrahisishia mtumiaji wa
huduma zenu na kurahisisha katika ukusanyaji wa mapato”, amesisistiza Eng.
Nyamhanga.
Naye, Kaimu Mtendaji
Mkuu wa TEMESA, Eng. Manase Ole Kujan amesema kuwa ukarabati wa kivuko hicho
umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 ambapo ukarabati mkubwa umefanyika
kwenye injini na mfumo wa umeme.
Eng. Kujan amefafanua
kuwa Serikali ina mpango wa kufanya upanuzi
wa eneo la kupumzikia abiria sehemu ya Kigamboni ambapo jumla ya nyumba 7 zitaathirika katika
mchakato huo.
“Nyumba hizi
zinaendelea kufanyiwa tathmini na taratibu za kuwalipa fidia zinaendelea”,
amesema Eng. Kujan.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni