Jumanne, 13 Septemba 2016

PROF. MBARAWA AKAGUA ATHARI ZA MIUNDOMBINU KAGERA



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kagera Eng. Andrea Kasamwa wakati alipokagua athari za tetemeko la ardhi lililoikumba miundombinu ya barabara mkoani humo.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Rwamishenye hadi Bandari ya Bukoba yenye urefu wa KM 4.6 ambayo imeathirika mita 60 kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mafundi wanaodhibiti eneo lililoathirika na tetemeko la ardhi katika barabara ya Bukoba-Mtukula yenye urefu wa KM 80 ambayo imeathirika kwa mita 200, mkoani Kagera.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amekagua athari za tetemeko la ardhi lililoikumba miundombinu ya barabara katika mkoa wa Kagera na kujionea athari zilizojitokeza katika mkoa huo.

Prof. Mbarawa amejionea athari za tetemeko la ardhi katika barabara ya Rwamishenye hadi Bandari ya Bukoba yenye urefu wa KM 4.6 ambayo imeathirika mita 60 na barabara ya Bukoba-Mtukula yenye urefu wa KM 80 ambayo imeathirika kwa mita 200 na kusisitiza kwamba Wizara yake itatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.

“Tunatoa pole kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kutokana na maafa yaliyojitokeza hivyo tutafanyia kazi maelekezo ya ukarabarati wa miundombinu iliyoathiriwa na tetemeko kadiri tulivyoelekezwa na Waziri Mkuu”, amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa yuko mkoani Kagera kukagua athari za uharibifu wa miundombinu kufuatia tetemeko la ardhi lililopiga mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza Septemba 10 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu takribani 16, majeruhi zaidi ya 100, uharibibifu wa nyumba takribani 800 na miundombinu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni