Muonekano
wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
|
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi
wanaozunguka eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kuwa
watulivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro
kati yao na mwendeshaji wa uwanja huo kampuni ya KADCO.
Prof
Mbarawa amesema ufumbuzi utakaopatikana utakuwa na manufaa kwa pande zote na
kujali maslahi ya Taifa.
"Msiwe
na wasiwasi Serikali yenu ni sikivu, tutayakagua maeneo yote na kuangalia
maslahi ya pande zote na kutoa maamuzi yenye manufaa kwa wote", amesisitiza
Prof. Mbarawa.
Mgogoro
kati ya wananchi wanaozunguka uwanja wa ndege wa KIA na kampuni ya KADCO ambao
umekuwako toka mwaka 1998 umesababisha misuguano na hisia kali kwa muda mrefu
hali iliyosababisha Serikali kuamua kuupatia ufumbuzi wa kudumu.
Waziri
Prof. Mbarawa ametuma timu ya wataalamu kupitia eneo lote la uwanja wa ndege
huo lenye kilomita za mraba 110 katika siku mbili kuanzia sasa ili kuangalia
wadau wote walioko ndani ya eneo hilo, athari zake kwa uwanja na wananchi kabla
ya kutoa uamuzi wa mwisho.
Amezungumzia
umuhimu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuilinda mipaka ya
viwanja vyake na wananchi kujiepusha kuvamia maeneo ya viwanja ili kuepuka
migogoro ya aina hiyo siku zijazo.
Katika
hatua nyingine Prof. Mbarawa ameitaka KADCO kuongeza mapato katika uwanja wa
ndege wa KIA ambao ni wa pili kwa ukubwa hapa nchini ili kuendana na kasi ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza mapato katika sekta zote za kiuchumi.
Amesema
nia ya Serikali ni kuboresha viwanja vyote vya ndege nchini ili kuimarisha
huduma ya usafiri wa anga.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KADCO Eng. Christopher Mukama amesema
KADCO inajiendesha kwa faida na kuhakikisha inaendelea na uboreshaji wa huduma
ili kuvutia ndege nyingi kutumia uwanja huo.
Waziri
Prof. Mbarawa yuko mkoani Arusha kukagua ujenzi wa miundombinu unaoendelea
mkoani humo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni