Jumanne, 4 Aprili 2017

BARABARA ZA ARUSHA KUKAMILIKA MWAKA HUU

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa uongozi wa Kampuni ya ujenzi ya Chicco, wakati alipokuwa akikagua barabara ya Kia-Mererani yenye urefu wa KM 26, mkoani Arusha, leo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akikaza nati katika daraja la Nduruma lenye urefu wa mita 60 linalojengwa katika barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1 wakati alipokagua barabara hiyo, mkoani Arusha leo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akikagua moja ya daraja lililopo katika barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1 inayojengwa na Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Hanil Jiangsu J/V wakati alipokagua barabara hiyo, mkoani Arusha leo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wakazi wa eneo la Sakina mkoani Arusha mara baada ya kukagua barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1 na barabara ya mchepuo (Arusha bypass) yenye urefu wa KM 42.4 na kumtaka mkandarasi M/S Hanil Jiangsu J/V anayezijenga kuhakikisha zinakamilika kwa wakati.

Barabara hizo ambazo zinajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 139.34 zina lengo la kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji la Arusha kwa kuwezesha magari makubwa kupita nje ya mji.

Aidha, Profesa Mbarawa amewataka wanachi wa mko wa Arusha kulinda miundombinu yote ya barabara hizo ili zidumu kwa muda mrefu na kuleta tija inayokusudiwa.

“Tunatumia pesa nyingi sana kujenga barabara hizi, hivyo nawaomba wananchi tuzilinde na tuzitunze ili zidumu kwa muda mrefu”, amesisitiza Profesa. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amewapongeza wajenzi na wasimamizi wa barabara hizo kwa hatua iliyofikiwa na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi na kuzingatia thamani ya fedha katika barabara hizo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Eng. Mgeni Mwanga, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara mkoani Arusha utakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

“Tumejipanga kuhakikisha barabara ya Sakina-Tengeru na ile ya mchepuo kukamilika kama ilivyopangwa ili kupunguza msongamano hali itakayovutia ongezeko la watalii na hivyo kukuza uchumi wa mkoa wa Arusha”, amesema Eng. Mwanga.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni