Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameridhishwa na
kasi ya ujenzi wa barabara ya Dodoma-Babati yenye urefu wa kilometa 188.15 ambayo
inajengwa kwa kiwango cha lami na kusisitiza kuwa ujenzi huo utakamilika mwezi
Oktoba mwaka huu.
Akizungumza
mkoani Manyara mara baada ya kukagua barabara hiyo, Waziri Prof. Mbarawa amewataka
Makandarasi M/S China Railyway Seventh Group anayejenga barabara ya Mela-Bonga
KM88.8 na M/S China Henan International Cooperation Group anayejenga barabara
ya Mayamaya-Mela Km 99.35 kuzingatia viwango vya ubora katika ujenzi wao kama
ilivyo kwenye mkataba, ili idumu kwa muda mrefu na kwa manufaa ya vizazi
vijavyo.
"Barabara
hii ni kiungo muhimu kwa mikoa ya Arusha, Manyara, Dodoma, Iringa na nchi za
Ukanda wa Afrika, hivyo naamini kukamilika kwake kutaibua fursa nyingi za
uchumi na kuchochea maendeleo ya wananchi", amesema Profesa Mbarawa.
Aidha,
Waziri Mbarawa amewataka wananchi wa mkoa wa Manyara na Dodoma kutumia fursa ya
kukamilika kwa barabara hiyo kujiendeleza kiuchumi na kuilinda ili iweze kudumu
kwa muda mrefu kwani ujenzi wake una gharama kubwa.
Kwa
upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Manyara, Eng.
Bashiru Rwesingisa na Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Eng. Salome
Kabunda wamemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa watawasimamia Makandarasi hao ili
kuhakikisha wanafanya kazi kwa ubora na kumalizika Oktoba mwaka huu kama
ilivyopangwa.
Barabara ya
Dodoma - Babati (km 188.15) inayojengwa kwa kiwango cha lami ni kiungo muhimu kwa
uchumi wa Tanzania, kwani inaunganisha nchi za bara la Afrika kutokea Capetown
(Afrika kusini) hadi Cairo (Misri).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni