Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa
reli ya kisasa (standard gauge) unatarajiwa kuanza mwezi Desemba mwaka huu na
kama ilivyo miradi mikubwa unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu na
utajengwa kwa awamu nne ili kuharakisha kukamilika kwake.
Waziri
Prof. Mbarawa amesema Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo leo, wakati wa Mkutano wa
Sita uliowakutanisha Mawaziri wa Sekta ya Uchukuzi wa nchi za Tanzania,
Rwanda na Burundi, uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesema lengo la
mkutano huo ni kuangalia namna bora ya kupunguza vikwazo kwenye sekta hiyo
baina ya nchi hizo.
Amesema
kuwa ushirikiano baina ya nchi za Afrika Mashariki katika ujenzi wa reli hiyo utachochea
kasi ya usafirishaji wa mizigo na shughuli za kibiashara na hivyo kuinua uchumi
wa nchi hizo.
“Kama
mnavyojua Serikali imetenga kiasi cha shilingi Trilioni moja kwa ajili ya
kuanza kutekeleza mradi huo na wenzetu nao watatafuta fedha katika nchi zao ili
kukamilisha ujenzi wake”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha
Prof. Mbarawa amebainisha kuwa kila nchi itatekeleza mradi wa kujenga reli ya
kisasa kwa sehemu yake hivyo ni wajibu wa kila nchi kukamilisha mradi huo ili
kuchochea maendeleo yanayotokana na Sekta ya Uchukuzi.
Amesema
kwa upande wa nchi ya Tanzania reli hiyo itaanza kujengwa kuanzia Dar es
Salaam-Tabora-Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa KM 1,219 ambayo ndiyo uti wa
mgongo wa reli yenyewe. Sehemu nyingine ni kutoka Tabora-Mpanda-Kalemela; Tabora-Uvinza
hadi Kigoma.
Katika
kuunganishwa na nchi ya Rwanda na Burundi, Waziri Mbarawa amesema ujenzi wa
reli hiyo itajengwa kuanzia Isaka-Rusumo mpaka Kigali na Keza mpaka Musongati.
Naye
Waziri wa Uchukuzi wa nchi ya Burundi Eng. Jeon Ntunzwenidana amefurahishwa na
Serikali ya Tanzania katika jitihada zake za kuharakisha ujenzi wa reli hiyo na
amesema Serikali ya Burundi itakamilisha ujenzi huo haraka ili kurahisisha
usafirishaji wa mazao na huduma za kibiashara baina ya nchi hizo.
Waziri
Prof. Mbarawa amesaini makubaliano ya uboreshwaji wa sekta ya mawasiliano, reli
na barabara baina ya nchi za Tanzania, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya
Demokrasia ya Congo (DRC).
Zaidi
ya trilioni 16 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa reli ya kisasa nchini Tanzania
yenye takribani urefu wa KM 2,600.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni