Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof.
Makame Mbarawa akibadilishana uzoefu na makapteni wa meli ya Azam aliposafiri
na boti hiyo.
|
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imejidhatiti
kufanya maboresho makubwa ya kimiundombinu na rasilimali watu katika sekta za
uchukuzi ili kuiwezesha sekta hiyo kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Prof. Mbarawa amesema
hayo mara baada ya kukagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na kusafiri wa
boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa ni mkakati wa kupata taarifa
sahihi kuhusu hali ilivyo sasa kutoka
kwa abiria na waendeshaji wa vyombo vya majini.
Amesema Serikali
itaboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kupunguza urasimu usio wa lazima na
kuwawezesha abiria na boti kukaguliwa kwa haraka na kuondoka kwa muda
unaotakiwa.
‘Tutahakikisha kuwa
idadi ya manahodha na wahandisi wa vyombo vya majini wazalendo inaongezeka ili
mkakati wa kuboresha usafiri wa majini hapa nchini uwiane na uwepo wa wataalam
wa uhakika’ amesema Prof. Mbarawa.
Waziri huyo wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano amesema Serikali ina mpango wa kujenga meli mpya za
kisasa katika Ziwa Victoria ili kuhamasisha wasafirishaji katika sekta ya
usafiri majini kuwa na vyombo vya kisasa na hivyo kupunguza gharama za usafiri.
Katika hatua nyingine
Prof. Mbarawa amekagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo amesisitiza
kuwa Serikali itaunga mkono juhudi zinazofanywa na Chuo hicho katika kutoa
mafunzo wa marubani wa ndege ili kuongeza idadi ya marubani wazalendo.
‘Mpango wetu wakukunua
ndege mpya unaendana na kuwezesha Chuo hiki chenye kufundisha marubani ili tuwe
na marubani wazalendo wa kutosha’ amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amewataka wafanyakazi
wa Chuo hicho kufanya kazi kwa uzalendo, ubunifu na kuzingatia matokeo ili
kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayokwenda haraka.
Naye Mkuu wa Chuo
hicho Profesa Zacharia Mganilwa amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa chuo
hicho kitashirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mamlaka ya Reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA), Kampuni hodi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) katika
kupata utaalam wa kisayansi katika mradi wa ujenzi wa reli ya kati ya Kisasa
kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Serikali imejipanga
kujenga chuo cha kisasa cha Usafirishaji kwa kushirikiana na Jamhuri ya Watu wa
China ikiwa ni mkakati wa kukifanya chuo hicho kuwa chuo mahiri katika upande
wa Afrika Mashariki na Kati.
Zaidi ya Shilingi trilioni
4 zimetengwa na Serikali katika bajeti ya mwaka huu ili kuimarisha miundombinu
ya usafiri wa Angani, barabarani, relini na majini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni