Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kulia mbele) akipata
maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), mkoa wa
Kagera Eng. Zephrine Bahyona (wa pili kushoto mbele), wakati alipokuwa akikagua
karakana yao na kuona changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
TTCL KUZALISHA
DOLA MIL 50.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameipa miezi
miwili Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), kuhakikisha kuwa inapata
Dola za Kimarekani milioni 50 ili kuongeza pato kwa Kampuni na Taifa kwa ujumla
kupitia Mkongo wa Taifa.
Akitoa
agizo hilo leo, wilayani Bukoba mkoani Kagera, Waziri Prof. Mbarawa amesema
agizo hilo limetokana na Serikali kuongeza masafa kwa kampuni hiyo kutoka 10
hadi 200 (MHZ) ambayo yana uwezo wa kuunganisha wateja wengi na wakubwa zaidi.
Amesisitiza
makampuni ya Simu nchini kuchangamkia fursa ili kupata masafa yenye uwezo
mkubwa kupitia mkongo huo.
"Hakikisheni
mnajipanga kuipata hiyo fedha ndani ya miezi miwili na kuwapatia masafa ya
kutosha wateja mlionao ndani na nje ya nchi na kujitahidi kuongeza wateja wengi
zaidi", amesema Prof. Mbarawa.
Aidha,
ameitaka TTCL kusogeza wigo wa kuwasiliana na wateja wakubwa ili
kuwashawishi kununua masafa hayo kulingana na mahitaji yao na hivyo
kutanua wigo wa kibiashara na kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida zaidi.
Kwa
upande wake Meneja wa TTCL mkoa wa Kagera Bw. Salum Mbaya amemhakikishia Waziri
huyo kuwa wataanza mara moja kazi ya kutembelea wateja wa ndani na nje ya nchi
kwa lengo la kuwapatia taarifa za ongezeko la uwezo wa mkongo na kuwashiwishi
kujiunga ili kupatiwa masafa wanayohitaji.
Bw.
Mbaya ametaja kuwa mpaka kufikia sasa nchi zilizounganishwa na mkongo wa
Taifa ni Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Kenya na Malawi.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mbarawa ametembelea uwanja wa ndege wa Bukoba na kuahidi
kutatua changamoto zinazoukabili uwanja wa ndege wa Bukoba ikiwemo kujenga jengo
la kuongezea ndege (Control Tower) ili kuongeza ufanisi na usalama katika
usafiri wa anga.
Naye,
Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini mkoa wa Kagera, Bi. Dorice Uhagile,
licha ya kuelezea mafanikio mbalimbali kama vile ongezeko la ndege na wateja uwanjani
hapo pia amefafanua changamoto mbalimbali zinazoukabili uwanja huo na kuiomba
serikali iweze kuwatatulia.
Waziri
Mbarawa ameanza ziara ya kikazi wilayani Bukoba, mkoani Kagera ambapo
ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara
yake.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni