Alhamisi, 18 Agosti 2016

SERIKALI YAJIPANGA KUBORESHA SEKTA YA UCHUKUZI






Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo kuhusu uboreshwaji wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Zacharia Mganilwa alipokagua chuo hicho jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akikagua moja ya darasa linalotumika kufundishia Marubani wa ndege alipokagua  Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na wanafunzi wanaosoma kozi ya udereva alipotembelea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam. Kushoto (mwenye tai nyekundu) ni Mkuu wa Chuo hicho Prof. Zacharia Mganilwa.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akibadilishana uzoefu na makapteni wa meli ya Azam aliposafiri na boti hiyo.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na mmoja wa abiria wanaotumia usafiri wa boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, na kujionea changamoto mbalimbali zinazowakabili abiria hao ambapo ameahidi kuzipatia ufumbuzi hivi karibuni.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imejidhatiti kufanya maboresho makubwa ya kimiundombinu na rasilimali watu katika sekta za uchukuzi ili kuiwezesha sekta hiyo kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Prof. Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na kusafiri wa boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa ni mkakati wa kupata taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo sasa kutoka  kwa abiria na waendeshaji wa vyombo vya majini.

Amesema Serikali itaboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kupunguza urasimu usio wa lazima na kuwawezesha abiria na boti kukaguliwa kwa haraka na kuondoka kwa muda unaotakiwa.

‘Tutahakikisha kuwa idadi ya manahodha na wahandisi wa vyombo vya majini wazalendo inaongezeka ili mkakati wa kuboresha usafiri wa majini hapa nchini uwiane na uwepo wa wataalam wa uhakika’ amesema Prof. Mbarawa.

Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amesema Serikali ina mpango wa kujenga meli mpya za kisasa katika Ziwa Victoria ili kuhamasisha wasafirishaji katika sekta ya usafiri majini kuwa na vyombo vya kisasa na hivyo kupunguza gharama za usafiri.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaunga mkono juhudi zinazofanywa na Chuo hicho katika kutoa mafunzo wa marubani wa ndege ili kuongeza idadi ya marubani wazalendo.

‘Mpango wetu wakukunua ndege mpya unaendana na kuwezesha Chuo hiki chenye kufundisha marubani ili tuwe na marubani wazalendo wa kutosha’ amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amewataka wafanyakazi wa Chuo hicho kufanya kazi kwa uzalendo, ubunifu na kuzingatia matokeo ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayokwenda haraka.

Naye Mkuu wa Chuo hicho Profesa Zacharia Mganilwa amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa chuo hicho kitashirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Kampuni hodi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) katika kupata utaalam wa kisayansi katika mradi wa ujenzi wa reli ya kati ya Kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Serikali imejipanga kujenga chuo cha kisasa cha Usafirishaji kwa kushirikiana na Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni mkakati wa kukifanya chuo hicho kuwa chuo mahiri katika upande wa Afrika Mashariki na Kati.

Zaidi ya Shilingi trilioni 4 zimetengwa na Serikali katika bajeti ya mwaka huu ili kuimarisha miundombinu ya usafiri wa Angani, barabarani, relini na majini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni