Jumanne, 10 Oktoba 2017

WAZIRI MBARAWA AWATAKA WAFANYAKAZI KUFANYA KAZI KWA UADILIFU



Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa amewataka wafanyakazi wote katika sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya kazi kwa uadilifu na ushirikiano katika kuwahudumia watanzania ili kufikia malengo ya Wizara.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo jana katika mapokezi ya Manaibu Mawaziri wapya wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Jijini Dar Es Salaam baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Dar es Salaam.

“Mimi nafurahi sana kufanya kazi katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa sababu mimi na wafanyakazi tuko katika timu moja; tunafanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano. Katika kipindi cha miaka miwili tumefanikiwa kufikia malengo mbalimbali ya serikali mfano ujenzi wa reli ya kisasa na barabara “ Mhe. Mbarawa amesema.

Akiwakaribisha Manaibu Mawaziri hao katika Wizara hiyo Prof. Mbarawa amesema yeye pamoja na wafanyakazi wote wa wizara wamefurahi kupata mawaziri wapya ambao watafanya nao kazi kwa pamoja katika wizara hiyo.

“Sisi kama viongozi tunapaswa kuwa mfano katika utendaji wetu wa kazi ili kujenga imani na umoja na wafanyakazi wetu, tunapaswa kufanya kazi kwa uadilifu, ushirikiano na umoja kwani haya ndio masuala ya msingi katika utendaji kazi,” Prof. Mbarawa amesema.

Kwa upande wake Naibu Waziri anayeshughulikia Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Atashasta Nditiye amesema kuwa amejipanga kufanya kazi na kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya nchi.

“Nipo tayari kufanya kazi itakayoleta mabadiliko, tutaboresha miundombinu ili kuchochea kasi ya ukuaji wa viwanda ,” amesema mhandisi Nditiye.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anaesimamia Sekta ya Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa  amesema atahakikisha anatumia vipaji vyake vyote katika kujenga umoja, uadilifu ili kufikia malengo ya sekta ya ujenzi.




Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Atashasta Nditiye (Wa pili kulia) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng. Joseph Nyamhanga (Kushoto) wakati alipokaribishwa katika ofisi za Wizara leo Jijini Dar es Salaam, Kulia ni Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho na Wa pili kushoto Katibu Mkuu Dkt. Maria Sasabo (Sekta ya Mawasiliano).


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawailiano, Prof. Makame Mbarawa (Kushoto), akisalimiana na Naibu Waziri Eng. Atashasta Nditiye (Kulia), wakati alipomtembelea Waziri Mbarawa ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi Dkt Leonard Chamuriho


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawailiano, Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akisalimiana na Naibu Waziri hiyo Mhe. Elias Kwandikwa wakati alipomtembelea Waziri Mbarawa ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (Katikati) akizungumza na Manaibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Atashasta Nditiye (Wa pili kulia) na Mhe. Elias Kwandikwa (Wa tatu kulia), wakati walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dar es Salaam,


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Atashasta Nditiye (aliyesimama) akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (Wa kwanza kulia), mara baada ya kuapishwa Jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe.  Elias Kwandikwa (aliyesimama) akieleza jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawailiano, Prof. Makame Mbarawa (Wa kwanza kulia), leo Jijini Dar es Salaam kabla ya kikao kazi na Makatibu Wakuu wa wizara na baadhi ya Watendaji waliopo jiji Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawailiano, Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akiwakabidhi manaibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Atashasta Nditiye (Kulia) na Mhe. Elias Kwandikwa wakati (Katikati) vitabu vya bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 ya Wizara hiyo kama mwongozo wa utendaji kazi mara baada ya kuapishwa jijini Dar es Salaam