Jumatatu, 8 Mei 2017

WANANCHI WAIOMBA SERIKALI KUKAMILISHA DARAJA LA SIBITI

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), mkoa wa Singida, Eng. Yohanes Mbegalo, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa kwanza kulia), kuhusu maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi wa Daraja la Sibiti lenye urefu wa M 82 linalounganisha Mikoa ya Singida, Simiyu, Manyara na Mara.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri Mr. Sunil Singh( Wa tatu kulia), anayesimamia mradi wa ujenzi wa Daraja la Sibiti lenye urefu wa M 82 na barabara za maingilio kwa kiwango cha changarawe KM 25, mkoani Singida jana.

Mhandisi Mshauri Mr. Sunil Singh, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (kulia), nguzo za Daraja la Sibiti zilizosimamishwa wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja hilo na barabara za maingilio kwa kiwango cha changarawe KM 25, mkoani Singida jana.


Muonekano wa nguzo za Daraja la Sibiti lenye urefu wa Mita 82 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 48. Daraja hilo ni kiungo muhimu kwani litaunganisha Wilaya ya Iramba na Mkalama mkoani Singida na Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Mwananchi Petro Daudi, kutoka Wilaya ya Meatu akimweleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa pili kulia), changamoto wanazozipata kipindi cha masika na kukosa mawasiliano na wenzao wa Wilaya nyingine jirani.

Mhandisi Mshauri Mr. Sunil Singh akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani kingo za Boksi Kalvati kubwa lililopo katika barabara za maingilio ya Daraja la Sibiti, mkoani Singida jana.

Muonekano wa Boksi Kalvati lililopo katika barabara za maingilio zinazoelekea katika Daraja la Sibiti KM 25 mkoani Singida.

Muonekano wa barabara ya maingilio kwa kiwango cha changarawe inayoelekea katika Daraja la Sibiti KM 25 mkoani Singida.

Wananchi wa kata ya Mpambala, wilaya ya Mkalama mkoani Singida wameiomba Serikali kuhakikisha inamaliza ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti haraka iwezekanavyo ili kurahisisha huduma za mawasiliano kati ya wilaya ya hiyo na mikoa jirani ya Simiyu, Manyara na Mara.

Wananchi hao wamemweleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, alipofika kukagua daraja hilo mkoani humo jana, ambapo pamoja na mambo mengine wamesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutatatua changamoto za usafiri hususan katika kipindi cha masika.

"Tunaomba Mheshimiwa Naibu Waziri utusaidie  kukamilisha daraja hili mapema ili  tupate huduma muhimu kama usafiri hasa kipindi cha masika", amesema mmoja wa wananchi. 

Aidha, wananchi hao wameipongeza Serikali kwa kuendelea na jitahada za ujenzi wa barabara za maingilio zenye urefu wa KM 25 katika daraja hilo ambapo kwa sasa mradi wote umefika asilimia 43.9.

Kwa upande wake Naibu Waziri Eng. Ngonyani ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani humo kuhakikisha kuwa wanamsimamia mkandarasi na kuhakikisha anamaliza ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara hizo kufikia mwezi Machi mwakani.

Kuhusu deni la mkandarasi huyo analoidai Serikali, Eng. Ngonyani amesema kuwa watahakikisha wanamlipa mapema ili kufanikisha mradi kumalizika kwa muda uliopangwa.
"Tutahakikisha tunalipa deni lote linalodaiwa ili kurahisisha mradi huu kuisha haraka kwa ajili ya wananchi kuweza kutumia daraja hili pamoja na barabara yake kwa kuwa ni kiungo muhimu kwao", amesisitiza Naibu Waziri.

Ametoa rai kwa wananchi wa maeneo hayo  mara tu mradi unapomalizika kuhakikisha wanalinda miundombinu yake kwani Serikali inatumia gharama kubwa katika utekelezaji wake.

Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoani humo, Eng. Yohanes Mbegalo,  amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwa atahakikisha mradi huo unaisha kwa wakati ili kuwaondolea wananchi kero ya usafiri.

Daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82 linajengwa na mkandarasi China Hanan ambalo linatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 16.
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni