Alhamisi, 4 Mei 2017

SERIKALI YATAKA MAKANDARASI NCHINI KUWAJIBIKA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikaribishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika moja ya banda lililopo katika ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Kikwete kabla ya kufungua Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), uliofanyika mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia), akikabidhiwa zawadi na mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni ya Denim Eleveators (kushoto) baada ya kukagua banda hilo katika ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), uliofanyika mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakiwa katika ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), uliofanyika mjini Dodoma.

Msajili wa Bodi ya Makandarasi Eng. Reuben Nkori akitoa taarifa ya kiutendaji kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), uliofanyika mjini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Makandarasi waliohudhuria  Mkutano wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), wenye kauli mbiu “Miaka 20 ya CRB Utendaji wa Makandarasi unaozingatia maadili na sheria kama mkakati wa kuaminiwa na waajiri”, uliofanyika mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Makandarasi waliohudhuria Mkutano wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), wenye kauli mbiu “Miaka 20 ya CRB Utendaji wa Makandarasi unaozingatia maadili na sheria kama mkakati wa kuaminiwa na waajiri”, uliofanyika mjini Dodoma.

Makandarasi wakisikiliza hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), wenye kauli mbiu “Miaka 20 ya CRB Utendaji wa Makandarasi unaozingatia maadili na sheria kama mkakati wa kuaminiwa na waajiri”, uliofanyika mjini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana (kushoto), wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), uliofanyika mjini Dodoma.


 Mwakilishi kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), akipokea tuzo kutoka kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), uliofanyika mjini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), na viongozi wengine wa Wizara katika ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa  mwaka wa CRB, uliofanyika mjini Dodoma.

Serikali imewataka Makandarasi kuwajibika na kufanya kazi zao kwa ufanisi na weledi ili kuishawishi Serikali kuwaamini na kuwapatia zabuni za kutekeleza miradi mikubwa nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), mjini Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa miradi mingi mikubwa nchini imekuwa ikitekelezwa na Makandarasi kutoka nje ya nchi hali inayopelekea Serikali kutumia fedha nyingi kuwalipa Makandarasi hao.

“Muda umefika sasa kwa makandarasi wazawa kuungana na kuomba zabuni za kutekeleza miradi mikubwa itakayowajengea uwezo kama ujenzi wa bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga, Reli ya Kisasa na miradi mingine”, amesema Makamu wa Rais.

Aidha, amefafanua kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo na Makandarasi wazawa kutaokoa fedha za ndani  za watanzania na hivyo kupelekea fedha hizo kubaki  nchini na vijana kupata ajira.

Sambamba na hilo Makamu wa Rais amewasisitiza Makandarasi hao kuwa wa kwanza kuomba zabuni pindi zinapotangazwa kwani Serikali ya Awamu ya Tano itatoa kipaumbele kwa Makandarasi wazawa wote nchini.

Makamu wa Rais ameitaka CRB kuhakikisha inasimamia Makandarasi hao kutekeleza miradi kwa muda uliopangwa pamoja na kufuata maadili katika utendaji wao wa kazi.

Kuhusu suala la ulipaji wa madeni ya Makandarasi Mhe. Samia Suluhu Hassan  amesema kuwa kwa sasa Serikali inendelea kufanya uhakiki wa madeni hayo ambapo zoezi la malipo litaanza mara baada ya uhakiki huo kukamilika. 

Kwa Upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa kutokana na umuhimu wa kuwathamini Makandarasi wazawa Wizara imetenga miradi maalum kwa ajili ya kuwajengea uwezo Makandarasi hao.

Profesa Mbarawa amewahakikishia makandarasi hao kupata fursa kwa zabuni zinazotangazwa na Wizara kwa kila Mkandarasi mwenye sifa atakayeomba zabuni hizo.
“Makandarasi msisite kuomba zabuni pindi zinapotangazwa, naahidi nitasimamia kwa uaminifu na kuhakikisha kila mkandarasi mwenye sifa anapata zabuni kwa mujibu wa sheria”, amesema Profesa Mbarawa.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini, Eng. Consolata Ngimbwa amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa watatumia mkutano huo kujadili changamoto zinazowakabili na hivyo kuja na mapendekezo sahihi ya kutatua changemoto hizo.

Mkutano huo wa siku mbili wenye kauli mbiu isemayo “Miaka 20 ya CRB, utendaji wa Makandarasi unaozingatia maadili na Sheria kama mkakati wa kuaminiwa na waajiri”  una lengo la kuwakutanisha  makandarasi wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili kwa pamoja changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni