Jumatano, 7 Desemba 2016

PROF. MBARAWA AITAKA BODI YA TCRA KUPATA MWAROBAINI WA WIZI WA MTANDAO

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa  akizungumza na wajumbe wa bodi mpya ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mara baada ya kuizindua rasmi, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jones Kilimbe (katikati), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, jjini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Faustine Kamuzora akizungumza na bodi, menejimenti na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), (hawapo pichani), wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani), alipoongea na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Eng. James Kalaba, wakifurahia jambo mara baada ya uzinduzi wa bodi mpya ya Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Bodi mpya ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakikisha wanapata mwarobaini wa kudhibiti ongezeko la wizi wa mitandao unaoendelea kukithiri hapa nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, Prof. Mbarawa amesema watanzania wameibiwa kwa muda mrefu kupitia njia ya ujumbe mfupi na kushawishiwa kutoa fedha kwa njia ya udanganyifu na hivyo kuitaka bodi hiyo kutofumbia macho changamoto hiyo.

“Changamoto ya wizi wa mitandao inagusa watanzania wengi, mkiwa na jukumu la kudhibiti mna wajibu wa kuwalinda wananchi”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa bodi hiyo ihakikishe inasimamia kwa karibu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika kudhibiti ubora wa masuala ya mawasiliano ikiwa ni teknolojia inayokuwa kwa kasi kubwa.

Aidha Prof. Mbarawa ameitaka bodi hiyo kuendelea kudhibiti wimbi la meseji za uchozezi zinazotumwa na baadhi ya wananchi kwa kukosa maadili.

Katika kuimarisha huduma ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini Waziri Prof. Mbarawa ameikata TCRA kufanya maamuzi ya haraka na kuwa wabunifu ili kuweka mazingira endelevu ya kukuza sekta hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Faustine Kamuzora amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ataisimamia bodi hiyo kwa kuzingatia ubora na kasi ya ukuaji wa teknolojia.

“Usipokuwa mbunifu katika sekta ya mawasiliano unaweza kujikuta unadhibiti teknolojia iliyopitwa na wakati hivyo ni lazima tuende sambamba na mabadiliko”, amesisitiza Prof. Kamuzora.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi mpya ya TCRA Dkt. Jones Kilimbe amesema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, Bodi itahakikisha inapata suluhu ya changamoto hizo ndani ya muda mfupi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni