Jumatatu, 10 Oktoba 2016

SERIKALI KUONGEZA MABEHEWA YA ABIRIA NA MIZIGO




Serikali imesema  itaongeza mabehewa ya abiria na mizigo katika Shirika la Reli la Tanzania (TRL), kwa lengo la kutatua adha ya usafirishaji kwa watumiaji wa reli ya kati  katika mikoa ya  Tabora, Kigoma na Katavi.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa uhaba wa mabehewa ya abiria umesababisha wananchi  wa maeneo hayo kutumia njia zisizo rasmi za ununuzi wa tiketi kwa ajili ya usafiri huo.

"Serikali imetambua changamoto kubwa ya usafiri inayowakabili wakazi wa mikoa hii, hivyo ni wakati muafaka kwa TRL kuongeza mabehewa matatu ili kupunguza adha ya usafiri", amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ameupongeza uongozi wa TRL kwa kuokoa matumizi ya zaidi ya Shilingi milioni 100 kwa kukarabati mabehewa ya mizigo 23 kwa kutumia wataalam wazawa wa shirika hilo.

Ameongeza kuwa Shirika hilo limetekeleza dhana ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza matumizi ya fedha na kuzingatia thamani ya fedha na kazi inayofanyika. 

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya ya kupunguza matumizi ya fedha mnazopata kwenye Shirika, ninaomba muendelee kutumia vyanzo vya ndani ili shirika lifikie hatua ya kujitegemea” amesema Profesa Mbarawa.

Naye, Meneja wa Usafirishaji wa TRL, mkoa wa Tabora Fredrick Masangwa ameiomba Serikali kuendelea na maboresho katika miundombinu ya reli kwa kiwango sawa na jinsi inavyoboresha miundombinu shindani ya barabara ili kuwepo na ushindani sawa katika sekta hizo mbili za usafirishaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Ndono-Urambo kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 52 na barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi na ukarabati wake.

Profesa Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo iende sambamba na viwango bora vya ujenzi wa barabara vilivyomo kwenye mikataba iliyosainiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abeli Busalama ameipongeza Serikali kwa juhudi za ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza fursa za kiuchumi katika wilaya yake na wilaya za jirani pamoja na mikoa inayozunguka wilaya hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Kaliua Mhe. Magdalena Sakaya amemuomba Waziri huyo kufikisha mawasiliano ya simu kwenye wilaya hiyo hususan vijijini ili kuweza kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Waziri Mbarawa amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili katika Mkoa wa Tabora ambapo amekagua miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, reli na mawasiliano.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni